Picha za satalaiti zilizochambuliwa na Le Monde zinaonyesha kuwa kambi ya kijeshi inayofadhiliwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) inajengwa huko Berbera, Somaliland, karibu na Lango-Bahari la Bab al-Mandeb.

Kazi ya ujenzi katika Uwanja wa Ndege wa Berbera, inayoendelea tangu Oktoba 2025, inaonekana kupanuka zaidi ya miundombinu ya raia, huku picha za satalaiti zikiashiria kuibuka polepole kituo cha kijeshi katika eneo hilo, kilichopo karibu na njia ya kusini kuelekea Bahari Nyekundu. Haya ni kwa mujibu wa uchambuzi uliochapishwa na gazeti la kila siku la Ufaransa, la Le Monde.

Kwa mujibu wa Le Monde, mradi huo unaofadhiliwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unaripotiwa hatimaye kuhudumia maslahi ya kimkakati ya Washington na Tel Aviv katika eneo hilo. Mamlaka ya Somaliland na Serikali ya Shirikisho ya Somalia huko Mogadishu hazijatoa maelezo yoyote kwa umma kuhusu madai hayo.

Thamani ya Berbera iko katika jiografia yake. Mji huo ambao uko kwenye Ghuba ya Aden karibu na Lango-Bahari la Bab al-Mandab, unaangalia korido ambayo ndiyo njia kuu ya usafirishaji wa biashara na nishati kati ya Asia na Ulaya.

Nafasi hiyo, kwa muda mrefu, imeufanya ufuo wa Pembe ya Afrika kuwa kivutio cha mataifa yanayoshindana yanayotaka kuwa na ushawishi wa kijeshi na kiuchumi katika eneo hilo; na ujenzi wa miondombinu unaoripotiwa unaoana zaidi na jitihada za madola ya kibeberu yanayotaka kuweka maguu yao huko Somaliland badala ya kuwa miundombinu ya maendeleo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Juni, Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, Abdul-Malik al-Houthi, aliapa kwamba atashambulia uwepo wowote wa Israel katika eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland kwa njia zote zinazowezekana, akisisitiza kwamba Yemen “haitakaa kimya mbele ya uwepo wowote wa Israel huko Somaliland, na haitawasubiri waoga.”

Sayyid Abdul-Malik al-Houthi alisema: “Tunafuatilia na kuchunguza kwa karibu hali ya Somaliland, na kile adui anachojaribu kufanya kwa kuigeuza kuwa uwanja wa kudhibiti Ghuba ya Aden, Lango Bahari la Bab al-Mandab na Bahari Nyekundu.”

Al-Houthi ameuhimiza Umma wa Kiislamu na nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu “kuchukua msimamo wa pamoja ili kumzuia adui kufikia malengo yake,” akisisitiza kwamba Yemen “itachukua hatua wakati wowote adui atakapoingia katika eneo hilo kwa kutumia nyenzo zote zinazopatikana.”

Israel ilitangaza kuitambua rasmi Somaliland kama dola huru mnamo Desemba 2025, hatua ambayo Somalia iliipinga na kuilaani vikali, ikiitaja kuwa ni “shambulio la makusudi dhidi ya mamlaka na uhuru wa Somalia.”

Aidha nchi za Afrika, Kiarabu na Kiislamu duniani zimepinga vikali hatua ya utawala wa Israel kuanzisha uhusiano na eneo la Somaliland ambalo ni sehemu ya Somalia.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *