Dar es Salaam.  Leo Julai 10, 2026 ni siku ya usikilizwaji wa shauri la kupinga uteuzi wa makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Shauri hilo la mapitio ya kimahakama (judicial review) limefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma na mwanaharakati Bubelwa Ephraim Bubelwa na mwenzake Joseph Daudi Mabugo.

Wamefungua shauri hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, na makamisha wake watatu.

Makamishna hao wa tume hiyo ambao pia ni walalamikiwa katika shauri hilo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.

Walifungua shauri hilo, Alhamisi Juni 18, 2026, baada ya kupata kibali cha Mahakama hiyo, kilichotolewa na Jaji Agustine Rwizile, Juni 8, 2026, baada ya kukubaliana na hoja za maombi ya walalamikaji hao kuwa wamekidhi matakwa ya kisheria kuruhusiwa kufungua shauri hilo.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa mahakamani hapo na Jaji Wilbert Chuma leo Julai 10, 2026.

Mara ya mwisho shauri hilo lilitajwa mahakamani hapo Juni 23, 2026 na Mawakili wa Serikali waliowawakilisha walalamikiwa wote wakaomba kupewa muda mfupi yaani siku tano tu badala ya siku 14 za kisheria kuwasilisha mahakamani hati ya majibu ya madai hayo pamoja na kiapo kinzani.

Mmoja wa mawakili wa walalamikaji, Hekima Mwasipu  aliomba baada ya walalamikiwa kuwasilisha majibu ya maandishi na kiapo kinzani dhidi ya madai hayo nao wapewe siku tano kuwasilisha majibu dhidi ya kiapo kinzani hicho cha walalamikiwa.

Japo mawakili wa Serikali walipinga ombi hilo, lakini Mahakama imekubalina na hoja za kiongozi wa jopo la mawakili wa waombaji, Mpale Mpoki kuwa walichokiomba kinaruhusiwa kwenye kanuni.

Hata hivyo, Jaji Chuma ameonya kuwa katika majibu ya kiapo hicho kinzani mawakili wa walalamikaji wasiibue mambo mapya ambayo hayakuwepo tangua hatua ya awali yaaombi ya kibali cha kufungua shauri hilo.

Kisha Mahakama hiyo iliwapa walalamikiwa siku tano za kuwasilisha majibu na kiapo kinzani kama walivyoomba kisha ikapanga kusikiliza shauri hilo leo.

Tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila, imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, na uteuzi wa  mwenyekiti makamishna wake ulitangazwa rasmi Mei 18, 2026.

Rais Samia ameunda tume kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Awali, kufuatia matukio Jeshi la Polisi liliwakamata watu kadhaa maeneo mbalimbali nchini na kuwafungua kesi mbali mbali za uhaini lakini baadaye Rais akaelekeza waachiwe.

Kisha Rais aliunda Tume ya Jaji Chande ambayo iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ambayo katika hotuba yake ya kukabidhi ripoti hiyo, watu 518 waliuawa na wengine kujeruhiwa, idadi ambayo alisema inaweza kuwa zaidi, ndipo baadaye akaunda tume hii ya Jaji Lila.

Hata hivyo, kabla tume hiyo haijaapishwa kuanza jukumu hilo, mwanaharakati Buberwa na mwenzake Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, wamekwenda mahakamani kuhoji uhalali wake.

Katika shauri hilo waombaji hao wanaiomba Mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa Rais Samia wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.

Sababu za kuomba kuipinga tume hiyo

Pamoja na mambo mengine walalamikaji wanapinga uamuzi wa Rais wa uteuzi wa makamishna hao wa tume hiyo wakidai kuwa Rais amefanya nje ya mipaka ya mamlaka yake ya kisheria na ni kinyume cha sheria.

Pia,wanadai kuwa hauna msingi wa kimantiki, unakwenda kinyume na matarajio halali ya waombaji na ya wananchi kwa jumla, unahusisha matumizi mabaya ya mamlaka ya hiari, na unapingana na masharti ya Katiba.

Hivyo, wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo leo, mawakili watakuwa katika mchuano mkali wa hoja za kisheria.

Mawakili wa walalamikaji watafafanua sababu za kupinga uteuzi wa makamishna hao kwa hoja za kisheria zikiungwa mkono na vifungu vya sheria iliyotumika kuunda tume hiyo na uteuzi wa makamisha wake, pamoja na kesi rejea mbalimbali kuishawishi Mahakama ikubaliane na madai yao.

Kwa upande wa mawakili wa walalamikiwa watakuwa na kibarua cha kupinga madai na hoja za mawakili wa walalamikaji, kwa hoja na vifungu vya sheria husika pamoja na kesi rejea mbalimbali kwa lengo la kuishawishi Mahakama ikubaliane na hoja zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *