
Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua rasmi dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa shahada ya kwanza katika taasisi za elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2026/27, huku ikiwataka waombaji kufuata taratibu zote zilizowekwa ili kuepuka usumbufu wakati wa kutuma maombi.
Dirisha hilo limefunguliwa ikiwa ni siku chache baada ya kutoka kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2026 huku asilimia 99.92 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Akitoa taarifa ya kufunguliwa kwa dirisha hilo, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema dirisha hilo limefunguliwa kuanzia leo Ijumaa Julai 10 hadi Agosti 10, 2026.
Profesa Kihampa amesema maombi yanawahusu makundi matatu ya waombaji ambayo ni wenye sifa za kuhitimu kidato cha sita, wenye sifa za stashahada (diploma) au sifa zinazolingana nazo, pamoja na wenye cheti cha awali (Foundation Certificate) cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Amesema waombaji wanapaswa kujiridhisha kuhusu vigezo vya kujiunga na programu wanazozitaka kwa kupitia kitabu cha mwongozo wa udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/27 kinachopatikana kwenye tovuti ya TCU pamoja na tovuti za vyuo husika.
“Tunawasihi waombaji kusoma kwa makini mwongozo wa udahili pamoja na maelekezo maalumu yanayotolewa na kila chuo kabla ya kuanza kutuma maombi,” amesema Profesa Kihampa.
Amesema waombaji wanatakiwa kutuma maombi moja kwa moja kupitia mifumo ya kielektroniki ya vyuo walivyovichagua badala ya kuwasilisha maombi kupitia TCU.
Aidha, amesema kila chuo kina maelekezo yake kuhusu namna ya kutuma maombi, hivyo waombaji wanapaswa kufuatilia taarifa hizo katika tovuti za vyuo husika.
Profesa Kihampa amesema waombaji wa Kitanzania wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani ya nje ya nchi wanapaswa kwanza kuthibitisha ulinganifu wa vyeti hivyo kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kwa vyeti vya elimu ya sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet) kwa vyeti vya stashahada kabla ya kuwasilisha maombi ya udahili.
Kwa upande wa waombaji wasiokuwa Watanzania wenye vyeti vya nje ya nchi, amesema watatakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja kupitia mifumo ya vyuo husika.
Pia, amewataka waombaji kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti rasmi ya TCU, tovuti za vyuo vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza na taarifa zinazotolewa na Tume kupitia vyombo vya habari.
Profesa Kihampa amewasisitiza waombaji wote wenye maswali kuhusu udahili kuwasiliana moja kwa moja na vyuo husika kwa masuala yanayohusu programu za masomo, huku masuala ya jumla yakielekezwa TCU.
Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na watu wanaojitambulisha kuwa mawakala au washauri wa kujiunga na vyuo vikuu, akisisitiza kuwa waombaji wanapaswa kutumia njia rasmi zilizowekwa ili kuepuka utapeli.