
Shirika moja la kutetea haki za binadamu na usimamizi wa michezo limetangaza mpango wake wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino, kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC). Shirika hilo linamtuhumu Infantino kwa kukiuka mara kwa mara sheria za kutofungamana na upande wowote katika masuala ya kisiasa, kupitia uungaji mkono wake wa wazi na uhusiano wa karibu na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Shirika la FairSquare, lenye makao yake makuu mjini London, limesema kuwa limeamua kuchukua hatua hiyo ya juu baada ya FIFA kutoonyesha ishara yoyote ya kuanzisha uchunguzi kufuatia malalamiko ya awali yaliyowasilishwa kwa Kamati yake ya Maadili mnamo Desemba 2025.
Shirika hilo limebainisha kuwa matamshi ya wazi ya Infantino na hatua zake za kumuunga mkono Trump zinaibua maswali mazito kuhusu iwapo anafanya hivyo kwa nafasi yake binafsi au kwa idhini ya uongozi wa FIFA. Imeelezwa kuwa hatua yoyote inayochukuliwa bila idhini rasmi inaweza kutafsiriwa kama matumizi mabaya ya mamlaka.
Aidha, FairSquare imetaja uamuzi wa Infantino wa kumtunza Trump Tuzo ya kwanza ya Amani ya FIFA (FIFA Peace Prize) kama sehemu ya malalamiko yake. Shirika hilo limeitaka FIFA kuchunguza iwapo uundaji wa tuzo hiyo na kukabidhiwa kwake kwa kiongozi wa kisiasa aliyeko madarakani unaendana na sheria za kutofungamana na siasa za shirikisho hilo.
Wakosaji wa tuzo hiyo wameelekeza kidole kwenye rekodi ndefu ya Trump ya ukiukaji wa haki za binadamu na maamuzi yenye utata, ikiwa ni pamoja na mizozo ya sera zake za kigeni, hatua kali dhidi ya wahamiaji, na kesi za kisheria zinazomkabili, kama sababu zilizofanya tuzo hiyo kukosolewa vikali.
Malalamiko hayo yameungwa mkono na wabunge 50 wa Bunge la Ulaya, huku Shirikisho la Mpira wa Miguu la Norway nalo likiunga mkono wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kimaadili.
Kesi hii inakuja huku kukiwa na ukosoaji mkubwa zaidi juu ya jinsi FIFA inavyoshughulikia masuala ya kisiasa yanayozunguka Kombe la Dunia la 2026, ikiwa ni pamoja na uamuzi wake wa kufuta adhabu ya kadi nyekundu kwa mchezaji wa mbele wa Marekani, Folarin Balogun, baada ya Trump kuripotiwa kuingilia kati suala hilo kwa kuzungumza na Infantino.
Aidha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mheshimiwa Masoud Pezeshkian, ameikosoa vikali Marekani kwa kutumia mashindano hayo kama jukwaa la kutoa shinikizo la kisiasa. Pia, Iran imelaani vikwazo na vizuizi vilivyowekwa dhidi ya timu yake ya taifa wakati wa mashindano hayo, ikieleza kuwa wachezaji wake walikabiliwa na vizuizi vya kusafiri ambavyo timu nyingine hazikukumbana navyo.