
Mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Shahidi Ayatullah Ali Khamenei, hayakuwa tukio la Iran pekee; bali pia uwepo mkubwa wa watu wenye ushawishi na wanablogu wa kigeni katika shughuli hiyo, wakiwemo Wamarekani ambao wamesema walikwenda Iran kuonyesha mshikamano wao na kutetea simulizi ya nchi hiyo mbele ya Marekani na Israel, umezusha hasira kubwa katika duru za Magharibi.
Gazeti la Times la London limemnukuu mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la Iran, Mohammad Mehdi Imani-Pour, akiliambia shirika la habari la Tasnim kwamba wanablogu wa kigeni wapatao 400 na watu wenye ushawishi walikuwa Iran kushiriki katika mazishi hayo.
Miongoni mwa waliohudhuria walikuwamo watu mashuhuri wa Marekani wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Jackson Hinkle ndiye aliyekuwa maarufu zaidi kati ya Wamarekani walioshiriki mazishi ya Ayatullah Khameni katika nchi za Iraq na Iran. Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 26 na mwenye ushawishi mkubwa katika mitandao ya kijamii alionekana kwenye jukwaa mjini Tehran, akiongoza nara na kaulimbiu kwa lugha ya Kiingereza zilizosema: “Down with the United States… Down with Zionism,” akiwa amebeba bendera nyekundu. Bendera hiyo, katika utamaduni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, ni nembo ya kulipiza kisasi.
Jackson Hinkle mwenye wafuasi karibu milioni nne kwenye mitandao ya kijamii, amekuwa akipinga siasa za kibeberu za Marekani, mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na sera za kikoloni za Magharibi kwa ujumla.
Christopher Hilali, pia ni miongoni mwa Wamarekani mashuhuri walioshiriki mazishi ya Ayatullah Khameni. Alikuwa mwanajeshi wa parachuti katika jeshi la Marekani, mwanaharakati, na mwanachama wa Chama cha Kikomunisti cha Marekani.
Hilali ameambia CNN kwamba: “Ilikuwa muhimu sana kwangu kuwa hapa katika wakati mgumu, kuonyesha mshikamano wangu na kusaidia kujenga umoja wa watu wa na taifa la Iran katika kukabiliana na ubeberu wa Marekani na Uzayuni.”
Pia alikuwepo mwanaharakati wa Marekani, Calla Walsh, ambaye hapo awali alijitolea katika kampeni ya urais ya Seneta wa chama cha Democratic, Elizabeth Warren; na katika miaka ya hivi karibuni amekuwa akipinga sera za Marekani na Israel.
Walsh alionekana mjini Tehran akiwa amevaa hijabu na kuiambia Press TV kwamba Ayatullah Ali Khamenei alikuwa “kiongozi wa watu wote wa dunia wanaopinga ubeberu, kiburi, Uzayuni na mauaji ya kimbari.”
Aliongeza kusema: “Kwangu mimi, Khamenei alikuwa kiongozi mkubwa zaidi wa kupinga ubeberu ambaye nimewahi kuona maishani mwangu.”
Mwandishi wa habari wa Marekani, Max Blumenthal, mwanzilishi wa tovuti ya “Grayzone”, pia alihudhuria mazishi ya Ayatullah Khameeni, na kuyataja mazishi hayo kuwa “makubwa zaidi katika historia.”
Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na watu mashuhuri wa Uingereza, miongoni mwao akiwa ni Bushra Shaikh, ambaye amesema ni “heshima kwake kuwa hapo ili kuangazia tukio hilo la kihistoria nchini Iran,” na Sakina Dato, ambaye alizungumzia hali ya “huzuni, hasira na ukakamavu” alioshuhudia Tehran.
Watu hao wenye ushawishi wameitaja Iran kuwa nchi yenye umoja na inayoweza kusimama kidete, na kumtaja Ayatullah Ali Khamenei kama nembo ya mapambano dhidi ya ushawishi wa Marekani na Israel.
Kuwepo Wamarekani hao wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kwenye mazishi ya kiongozi Shahidi wa Iran kumeibua hasira miongoni mwa watu walio karibu na Rais Donald Trump. Gazeti la The Times limeripoti kwamba, Sebastian Gorka, naibu msaidizi wa rais wa Marekani, ametuma maoni kwenye mtandao wa X akikariri sheria ya uhaini ya Marekani, huku kukiweko wito wa kufunguliwa mashtaka dhidi ya Wamarekani walioshiriki kwenye shughuli hiyo ya kihistoria nchini Iran.