Tanga. Serikali imetangaza mpango wa kujenga gati jipya lenye urefu wa mita 300 katika Bandari ya Tanga kufuatia ongezeko la shehena ya mizigo na mapato, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia meli na mizigo inayozidi kuongezeka.
Akizungumza leo Jumatatu, Julai 13, 2026 jijini Tanga baada ya kukagua maendeleo ya bandari hiyo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Amesema ujenzi wa gati hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha uchumi kupitia sekta za usafirishaji, biashara na nishati.
“Serikali inaendelea kupanua Bandari ya Tanga ili iendane na mahitaji yanayoongezeka ya usafirishaji wa mizigo na kuifanya kuwa kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa nchi,” amesema Balozi Omar.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Bandari ya Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya bandari hiyo. Picha na Mbonea Herman.
Mbali na upanuzi wa bandari, amesema Serikali imepanga pia kuboresha miundombinu mingine ya usafirishaji katika mwaka huu wa fedha, ikiwemo reli na uwanja wa ndege wa Tanga, ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria.
Amesema ujenzi wa barabara ya kimkakati ya Tanga – Pangani yenye urefu wa kilomita 50 unatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa Mkoa wa Tanga.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa barabara ya Handeni–Singida, kama ulivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kuimarisha muunganiko kati ya Bandari ya Tanga na maeneo ya ndani ya nchi, hatua itakayoongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo.
Hata hivyo, Waziri Omar amewapongeza viongozi na watendaji wa Mkoa wa Tanga pamoja na TPA kwa kusimamia maboresho ya Bandari ya Tanga yaliyogharimu Sh429.1 bilioni.
Amesema ndani ya mwaka mmoja tangu kukamilika kwa maboresho hayo, bandari imekusanya mapato ya Sh436 bilioni, hali inayoonyesha kuwa uwekezaji huo umeanza kuleta matokeo chanya kwa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega amesema maboresho yaliyofanyika yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia mizigo, ambapo shehena imeongezeka kutoka tani 750,000 hadi kufikia tani milioni 2.7.
Mbega amesema pia makusanyo ya mapato ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka Sh31 bilioni hadi Sh298.7 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/26.
Kutokana na ongezeko hilo la shughuli za bandari, amesema Bandari ya Tanga imeanza kuzidiwa na idadi ya meli na shehena ya mizigo, hivyo TPA imepanga kujenga gati jipya katika mwaka wa fedha 2026/27 pamoja na gati maalumu la kuhudumia mafuta na meli za makontena ili kuiongezea uwezo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batlida Burian amesema tayari mkoa umetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kuhifadhi mafuta (Oil Terminals).
Amesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa nishati, kuvutia wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda na biashara mkoani Tanga.