
Dar es Salaam. Baraza la Famasi limesitisha leseni za wanataaluma sita wa kada ya famasi baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka sheria, kanuni, miiko na maadili ya taaluma huku wengine sita wakipewa onyo kali kufuatia makosa mbalimbali ya kitaaluma.
Baraza hilo, ambalo ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya yenye jukumu la kusimamia taaluma ya famasi nchini, limetoa uamuzi huo baada ya kikao chake cha 60 kilichofanyika Juni 4 na 5, 2026, ambapo lilijadili mashauri mbalimbali yaliyowasilishwa na Kamati ya Nidhamu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Baraza la Famasi, Julai 10, 2026 wanataaluma hao walipatikana na hatia ya kukiuka masharti ya Sheria ya Famasi, Sura ya 311 na kanuni za miiko na mwenendo wa kitaaluma kwa wanataaluma wa kada ya famasi za mwaka 2024.
Makosa yaliyobainika ni pamoja na kufanya udanganyifu katika utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma kwa kuingia mikataba ya usimamizi na utoaji wa huduma za dawa kinyume cha utaratibu.
“Makosa mengine ni kutoa huduma za kitabibu zisizoruhusiwa kisheria katika maduka ya dawa, kushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu ya usimamizi wa famasi, pamoja na kuruhusu huduma za dawa kutolewa na watu ambao hawajasajiliwa na Baraza la Famasi,” taarifa hiyo imeeleza.
Makosa mengine ni kuwasilisha taarifa za udanganyifu kwa Ofisi ya Msajili kuhusu vigezo vya majengo yaliyokusudiwa kusajiliwa kwa ajili ya utoaji wa huduma za famasi, pamoja na kuwasilisha taarifa za uongo kwa lengo la kupata usajili wa awali.
Baada ya kusikiliza na kupitia ushahidi wa mashauri yote, Baraza liliwakuta wanataaluma 12 na hatia ya ukiukaji wa sheria, kanuni, miiko na maadili ya taaluma ya famasi. Kati yao, sita wameadhibiwa kwa kusitishiwa leseni zao za kitaaluma, huku sita wengine wakipewa onyo.
Wakati huohuo, Baraza hilo limesema wanataaluma wawili waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali hawakupatikana na hatia baada ya ushahidi uliowasilishwa kutokuthibitisha madai dhidi yao.
Baraza la Famasi limekumbusha wanataaluma wote wa kada ya famasi kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma katika utoaji wa huduma ili kulinda usalama wa wananchi na kuendelea kudumisha hadhi ya taaluma hiyo nchini.