Geita. Bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Kalangalala, iliyopo Manispaa ya Geita, limenusurika kuteketea baada ya moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika kuzuka na kuunguza kitanda kimoja pamoja na baadhi ya mali za wanafunzi.

Tukio hilo limetokea leo Julai 13, 2026 saa 6:30 mchana wakati wanafunzi walipokuwa wakiendelea na masomo darasani.

Moto huo ulibainika baada ya wanafunzi kuona moshi ukitoka katika bweni hilo linalokaliwa na wanafunzi 96.

Makamu Mkuu wa shule hiyo Antidius Deusdedit ameliambia Mwananchi kuwa walimu walipokea taarifa za moto huo kutoka kwa wanafunzi na kuchukua hatua za haraka huku wakiwasiliana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Tulikimbilia eneo la tukio na kuanza kupambana na moto kwa kutumia vizima moto pamoja na ndoo za mchanga kabla ya askari wa zimamoto kufika,” amesema Deusdedit.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakihamisha kitanda kilichoteketea kwa moto kutoka bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Kalangalala, Manispaa ya Geita, baada ya tukio la moto. Picha na Chubwa.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Yusuf Zacharia   amesema moto huo uligunduliwa na mwanafunzi aliyekuwa amekaa karibu na dirisha darasani.

“Tulikuwa darasani tunaendelea na masomo. Mwanafunzi aliyekuwa dirishani aliona moshi na kumjulisha mwalimu. Tulielekezwa kwenda kuuzima moto, tukachukua ndoo za mchanga na kuumwaga kwenye moto hadi ukazimika,” amesema.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Keneth Mwakasitu amesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha moto huo, huku dalili za awali zikionyesha huenda ulisababishwa na uzembe wa kibinadamu.

Amesema hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa kutokana na tukio hilo, kwa kuwa lilitokea wakati wanafunzi wote wakiwa madarasani.

“Madhara yaliyotokea ni madogo. godoro moja na chandarua kimoja vimeteketea. Pia baadhi ya madaftari ya wanafunzi, ndoo, vikombe, balbu zilizoharibiwa na joto pamoja na kioo cha dirisha vimeharibika,” amesema Mwakasitu.

Amesema kiwango kidogo cha uharibifu kimetokana na mwitikio wa haraka wa walimu na wanafunzi pamoja na elimu ya kujikinga na majanga ya moto ambayo Jeshi la Zimamoto limekuwa likiitoa shuleni hapo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *