
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea hatua za kichokozi za utawala wa Marekani kuwa ni ukiukaji wa makubaliano ya Islamabad na chanzo cha mgogoro unaohusu utekelezaji wake.
Esmaeil Baghaei amesema: “Hakuna shaka kwamba makubaliano ya Islamabad yameingia katika hali ya mgogoro; hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kukiuka ahadi zake, bali ni Marekani ndiyo imekuwa ikikiuka mara kwa mara wajibu wake.”
Kauli hii ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ndio ufunguo unaofafanua sababu hasa ya kuingia Makubaliano ya Islamabad katika hatua ya mzozo. Makubaliano hayo yalikusudiwa kuweka mfumo maalum, baada ya kumalizika vita, kwa ajili ya kupunguza mivutano, kuimarisha usitishaji vita na kuzuia kuzuka upya mapigano, lakini kwa bahati mbaya, hali ya mambo imeingia katika hatua nyeti kutokana na “ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano hayo unaofanywa kwa makusudi na Marekani.” Kwa miaka mingi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha wazi nia yake njema katika utekelezaji wa wajibu wake wa kimataifa. Akisisitiza rekodi hiyo nzuri, Baghaei amesema “hakuna anayeweza kuituhumu Iran kuwa imekiuka ahadi zake.” Hata hivyo, kilichopelekea makubaliano ya Islamabad kuingia katika mzozo hakikutokana na kasoro yoyote upande wa Iran, bali ni “kuharibiwa” na Wamarekani vipengele vya makubaliano hayo yenye nukta 14.
Tangu mwanzo, Iran imejenga msimamo wake juu ya kanuni ya “ahadi kwa ahadi,” ambapo pale upande wa pili unapotimiza wajibu wake, Tehran nayo inatekeleza ahadi zake bila kusita. Hivyo, kwa mtazamo wa mfumo wa kidiplomasia wa Iran, mgogoro wa sasa si suala la kisheria bali ni mgogoro wa kutoaminiana ambao unaotokana na historia ndefu ya Washington kukiuka ahadi zake. Moja ya hoja kuu zenye utata ni Ibara ya 5 ya Hati ya Makubaliano ya Islamabad, inayohusu usimamizi wa usalama katika Lango Bahari la Hormuz. Baghaei anasisitiza kuwa ibara hiyo iliandaliwa kwa usahihi na uwazi mkubwa kiasi cha kutotoa mwanya wowote kwa Marekani kufanya “tafsiri ya kimaslahi.”
Lengo la kifungu hiki lilikuwa kuanzisha utaratibu wa pamoja, kwa mashauriano na Oman, ili kuhakikisha usalama wa urambazaji, huku ukizuia kutumiwa vibaya kijeshi Lango-Bahari la Hormuz dhidi ya Iran. Baghaei imesema kwamba Washington, kwa kuwashinikiza baadhi ya wahusika wa kikanda na kuunda mifumo sambamba, imezuia utekelezaji wa kifungu cha tano na hata kuhimiza au kulazimisha meli kuzima mifumo yao ya urambazaji, hatua ambayo imeongeza hatari ya ajali za meli baharini, matukio ya kimazingira na kukosekana usalama wa kutosha katika njia za maji za kimataifa.
Kipengele kingine muhimu cha matamshi ya Baghaei ni kufichuliwa kwa uzushi wa maafisa wa Marekani kuhusu mazungumzo ya Muscat. Amesema waziwazi kwamba: “Uongo umekuwa sehemu ya tabia ya mfumo wa utawala wa Marekani; ambapo wamezoea hali hiyo kupita kiasi.” Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amekanusha madai ya Trump kwamba Iran ilikubaliana na kila kitu huko Muscat kisha ikashambulia meli, akisisitiza kuwa hakuna ukweli wowote katika madai hayo. Mazungumzo ya Muscat yalijikita katika suala la Lango la Hormuz pekee na yalifanyika ndani ya mfumo wa Kipengele cha 5 cha Makubaliano ya Islamabad. Iran, kwa kushauriana na Oman, ilibuni utaratibu wa kudhamini usalama wa meli katika eneo hilo, lakini “mashinikizo ya wazi na ya siri ya Marekani dhidi ya Oman” yamekwamisha juhudi hizo. Uingiliaji huu unathibitisha kuwa Marekani haitaki kufikia usalama wa kikanda bali imedhamiria kuendeleza hali ya ukosefu wa usalama katika eneo.
Mgogoro unaohusu utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano ya Islamabad haukomei tu kwenye suala la Lango la Hormuz. Kuhusu suala hili, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mfululizo wa vitendo vya Marekani, ikiwa ni pamoja na mashinikizo ya kijeshi yanayoongezeka, vikwazo na hatua za upande mmoja, vimetilia shaka mantiki halisi ya mazungumzo hayo.
Ikiwa upande mmoja wa makubaliano unatumia zana za kijeshi, mashinikizo ya kisiasa na hatua za kulazimisha matakwa yake dhidi ya upande mwingine kwa wakati mmoja, mtu hawezi tena kuzungumzia uwepo wa mazungumzo thabiti na endelevu.
Kwa mtazamo wa Tehran, licha ya kuwa Mazungumzo ya Islamabad bado hayajavunjika kabisa lakini yamefikia hatua ambayo uhuishwaji wake unategemea mabadiliko ya tabia ya Marekani na utekelezaji wa ahadi zake. Usalama wa Lango Bahari la Hormuz unapasa kudhaminiwa na mataifa ya Ghuba ya Uajemi kupitia mifumo ya kikanda, si kwa uwepo wa vikosi vya nje ya kanda ambavyo vyenyewe ni chanzo kikuu cha kuvurugwa usalama wa eneo hili. Kwa maelezo hayo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kwamba makubaliano hayo yatabaki kuwa endelevu iwapo tu kanuni ya “ahadi kwa ahadi” itazingatiwa na kutekelezwa kivitendo. Kwa mtazamo wa vyombo vya kidiplomasia vya Iran, ikiwa upande mmoja utavunja masharti ya makubaliano na kutarajia upande wa pili utekeleze kikamilifu majukumu yake, matokeo yake bila shaka yatakuwa ni kutumbukia makubaliano hayo kwenye mgogoro. Kwa msingi huo, huku ikisisitiza msimamo wake wa kutatulia kidiplomasia mgogoro uliopo, Tehran imeshurutisha kurejea kwa Makubalianbo ya Islamabad katika njia yake ya kawaida na kukomeshwa tabia ya Marekani ya kuyakiuka mara kwa mara na wakati huo huo kutimiza kikamilifu majukumu yake, sharti ambalo ndiyo njia pekee ya kuepuka mgogoro unaoongezeka na kurejesha utulivu katika eneo.