Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongofleva, Linah a.k.a Ndege Mnana, ni miongoni mwa wanamuziki waliotoka chini ya usimamizi wa Tanzania House of Talent (THT), takribani miaka 15 iliyopita huku wengi wakimtabiria kufika mbali.
Hata hivyo, kwa sasa Linah ni kama ameamua kususa kurekodi nyimbo zake binafsi ikiwa ni miaka zaidi ya miwili bila kuachia wimbo mpya, kitu ambacho si cha kawaida kwa mwanamuziki wa daraja lake.
Inaelezwa kuwa Linah alianza kuimba muziki kanisani kisha baadaye sana ndipo akaibukia katika muziki wa kidunia (secular artist) kama ilivyokuwa kwa mastaa kama Celine Dion na marehemu Whitney Houston.
Nyimbo za mwanzoni kumpatia Linah mashabiki na hata umaarufu ni Atatamani (2010), Bora Nikimbie (2010) na Lonely (2011), ambazo zilifanya vizuri katika chati mbalimbali za redio nchini.
Kufanya vizuri kwa nyimbo hizo kulipelekea kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2011 akipokea kijiti hicho kutoka kwa Diamond Platnumz aliyeshinda msimu wa 2010.
Linah aliwania kipengele hicho kupitia wimbo wake, Atatamani (2010) ambao ulitayarishwa na Duke Tachez na Mosse chini ya M Lab, studio ambayo imewatoa mastaa wengi akiwemo Ben Pol.
Ushindi huo ulikuja baada ya kuwabwaga washindani wake ambao ni Sam wa Ukweli (Sina Raha), Sajna (Iveta), Bob Junior (Oyoyo), na Top C (Lofa). Vilevile kati 2012 hadi 2025, Linah alitajwa kuwania TMA katika kipengele cha Msanii Bora wa Kike.
Baadaye alikuja kufunika zaidi kupitia wimbo wake, Ole Themba (2014) ambao video yake iliyofanyika Afrika Kusini chini ya usimamizi wa Godfather na inatajwa kugharimu Dola40,000, wastani wa Sh105 milioni kwa sasa.
Inaelezwa kuwa wimbo huo uliotengenezwa na Uhuru kutoka Afrika Kusini, ulipaswa kuwa sehemu ya wimbo wa Davido na Mafikizolo, Tchelete (2014) ila ikashikana hivyo kila mmoja ukatoka kivyake.
Hivyo Linah katika kipindi chake cha mwanzoni hakuanza kinyonge, nyota yake iliangaza mapema na kwa miaka mingi aliendelea kufanya vizuri lakini kwa sasa amekuwa kimya kimuziki kwa muda mrefu.
Wimbo wa mwisho Linah kuachia unaitwa ‘Nyota’ ambao ulitoka Desemba 2023 ukiwa umetayarishwa na Jini x66, mtayarishaji muziki ambayo ametengeneza nyimbo nyingi maarufu za Jay Melody.
Linah anaungana na wasanii wenzake wa kike ndani ya Bongofleva ambao wameamua kukaa kimya kimuziki, baadhi yao ni Queen Darleen, Hamisa Mobetto na Recho Kizunguzungu.
Queen Darleen, msanii wa zamani wa WCB Wasafi, mara mwisho kutoa wimbo ilikuwa Machi 11, 2020 alipoachia ngoma yake ‘Bachela’ akimshirkisha Lava Lava huku Abby Dady na Rash Don wakihusika katika utayarishaji.
Naye Hamisa Mobetto, Miss XXL After School Bash 2010, amekuwa kimya tangu alipoachia Extended Playlist (EP) yake, Your Truly (2022), hivyo sasa imetimia miaka minne tangu aliposikika katika Bongofleva kwa mara ya mwisho.
Kwa upande wake Recho Kizunguzungu ambaye naye alitoka kupitia THT, ana miaka miwili bila kuachia ngoma mpya, mara ya mwisho alifanya hivyo Julai 2024 akitoa wimbo wake ‘Saizi Yangu’ akimshirikisha Stamina.
Mbali na muziki, pia Linah amekuwa kimya katika mitandao ya kijamii, mathalani ameondoa post nyingi na kubakisha tatu pekee katika ukurasa wake wa Instagram ambao una wafuasi zaidi ya milioni 6.6.
Chapisho la mwisho ambalo limesalia katika ukurasa huo, liliwekwa Mei 9, 2023. Chapisho lilikuwa na ujumbe uliosomeka: Kila mara naleta mwonekano wa kuvutia na wa kujiamini kwenye Instagram.
Katika nyakati hizi ambazo wasanii wanatumia mitandao ya kijamii kutangaza kazi zao, Linah yeye amechagua njia tofauti na wenzake.
Utakumbuka Linah anashika nafasi ya sita kati ya wasanii wa kike wa Bongofleva wenye wafuasi wengi katika mtandao wa Instagram akiwa ametanguliwa na Hamisa Mobetto, Shilole, Nandy, Vanessa Mdee na Zuchu.