Kigoma. Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara ya siku moja mkoani Kigoma Julai 20, 2026, ambapo atazindua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway – SGR), kipande cha sita (Lot 6) kutoka Tabora hadi Kigoma.

Mradi huo wenye urefu wa kilometa 506 na thamani ya Sh6.31 trilioni unatekelezwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) chini ya usimamizi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 10.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 17, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Simon Sirro, alisema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa haraka, usalama na gharama nafuu, sambamba na kufungua fursa mpya za kiuchumi.

“Utekelezaji wa mradi huu utawezesha usafirishaji wa haraka, salama na wenye gharama nafuu wa mizigo na abiria. Pia utafungua fursa za biashara, uwekezaji na utalii kwa Mkoa wa Kigoma na nchi jirani za Ukanda wa Maziwa Makuu,” alisema Sirro.

Mbali na uzinduzi wa mradi wa SGR, Rais Samia pia anatarajiwa kuzindua ujenzi wa meli nne mpya zinazojengwa mkoani Kigoma kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri katika Ziwa Tanganyika.

Meli hizo zinatarajiwa kuboresha usafiri wa majini, kuongeza usalama wa wasafiri na kuchochea shughuli za biashara na uchumi kwa wananchi wa Tanzania na nchi jirani zinazotumia ziwa hilo.

Katika ziara hiyo, Rais Samia atapata pia taarifa ya maendeleo ya ukarabati wa meli kongwe ya MV Liemba, ambayo imehudumu kwa zaidi ya miaka 100. Kwa sasa, ukarabati wa meli hiyo umefikia asilimia 90 tangu iliposimamisha safari zake mwaka 2023.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 8, 2026 na Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL), MV Liemba imepandishwa kwenye chelezo (slipway) kwa ajili ya kukamilisha kazi za sehemu ya chini ya meli, ikiwemo kufungwa propela (propeller), shafti, pamoja na kupakwa rangi sehemu ya chini ya meli.

Ukarabati wa MV Liemba unafanywa na kampuni ya M/S Brodosplit JSC ya Croatia kwa kushirikiana na Dar es Salaam Merchant Group (DMG), ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *