Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewaomba Watanzania kuchangia katika huduma za afya ili kuwasaidia wenye matatizo na uhitaji wa matibabu na kwamba utamaduni wa kusaidia uwe endelevu.

Dk Mwigulu alitoa kauli hiyo usiku wa kuamkia leo Julai 17, 2026 wakati akiongoza harambee ya uchangiaji wa matibabu ya huduma za afya kwa magonjwa ya figo na upandikiza uroto kwa watoto iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT).

Wanawake hao waliandaa kongamano hilo wakilenga kuchangia Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kuisaidia Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa ambayo imelenga kutafuta Sh7 bilioni kwa ajili ya kuwasaidia wasiojiweza katika magonjwa ya figo na upandikizaji wa uroto.

“Tanzania ni lazima tufikie hadhi ya kuwa rufaa kwa nchi zingine, watu waje kwetu kupata matibabu lakini tunahitaji watu wetu kuwa na afya njema, naomba watu wasisite kuchangia kwenye mambo haya kwani yanakwenda kuwa msaada kwa watu wetu,” amesema Dk Mwigulu.

Kwenye kongamano hilo, zaidi ya Sh2.2 bilioni zilikusanywa ikiwemo fedha taslimu na ahadi ambapo Ofisi ya Rais wamechangia Sh50 milioni wakati Ofisi ya Waziri Mkuu wakichangia Sh30 milioni na hivyo jumla ya michango yote ilisaidia kuvuka lengo lililokusudiwa.

Awali, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema kuna watoto 50 wanaosubiri huduma za upandikiza uroto na wengine 50 wako kwenye foleni ya kusubiri huduma za matibabu ya figo ambapo matibabu ya magonjwa hayo yana gharama kubwa.

Profesa Makumbi amesema huduma ya upandikizaji uroto kwa mtoto mmoja ni Sh75 milioni ambapo idadi ya watoto hao itabidi walipie Sh3.75 bilioni huku huduma za matibabu ya figo kwa mgonjwa ni Sh40 milioni na kwa wagonjwa 50 itabidi walipie Sh2 bilioni ambazo kwa ujumla wake zitatakiwa Sh5.75 bilioni.

Mkurugenzi huyo anasema huduma za magonjwa hayo ni za juu lakini haziwezi kufikia gharama ambazo wangezilipa kama wangepata huduma za matibabu kwa nchi zingine walikokuwa wakipelekwa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa sasa imekuwa ni kimbilio la nchi jirani akieleza huduma za hivi karibuni ambapo wamewahudumia watoto kutoka Burundi waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo ya moyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda amesema uamuzi wa kuanzisha harambee hiyo ulitokana na ukweli kuwa mahitaji yanayotakiwa yana msingi kwani mateso ya Watanzania yamekuwa ni makubwa katika magonjwa hayo kutokana na kipato.

“Mtoto mmoja katika upandikizaji uroto akipelekwa nje anatakiwa kulipiwa Sh120 milioni wakati Tanzania ni Sh75 milioni na kwa mgonja wa figo nje ya nchi angelipiwa Sh90 milioni, sasa tulipoona hili tukasema ni lazima nasi tuguswe,” amesema Chatanda.

Chatanda amesema mkakati huo wataendelea nao kuanzia sasa na utakuwa ni endelevu wakiwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi ili ndoto ya Hospitali ya Benjamini Mkapa katika kuwahudumia wagonjwa ifikiwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *