
Leo ni Jumamosi 3 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria mwafaka na 18 Julai 2026 Miladia
Miaka 1391 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Mwezi 3 Safar mwaka 57 Hijria Qamaria, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, alizaliwa Imam Muhammad Baqir (AS), mjukuu kipenzi wa Bwana Mtume SAW katika mji wa Madina. Ukamilifu wa kiroho na kielimu ambayo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu waliyotunukiwa Ahlubaiti wa Mtume SAW, ulidhihirika kwa uwazi katika shakhsia ya Imam Muhammad Baqir (AS). Katika kipindi cha miaka 19 ya Uimamu wa mtukufu huyo, ambacho kilisadifiana na miaka ya mwishoni ya utawala wa Bani Umayyah, yalipatikana mazingira mwafaka katika jamii kwa yeye kuweza kuimarisha misingi ya kifikra na kiutamaduni ya Waislamu. Taaluma nyingi zilistawishwa na kuenea katika jamii ya Waislamu kupitia chuo cha fikra cha mtukufu huyo pamoja na mwanawe, yaani Imam Ja’far Sadiq (AS); na hata wanafunzi wake walikuja kuwa wavumbuzi wa taaluma mbalimbali mpya za elimu. Lakini sambamba na hayo, Imam Baqir hakughafilika na kupambana na dhulma na uonevu wa utawala wa kidhaliimu wa Bani Umayyah na ndiyo maana katika mwaka 114 Hijria Qamaria aliuliwa shahidi na mtawala wa zama hizo. Tunachukua fursa hii pia kukupeni mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa kwa mjukuu huyo kipenzi wa Mtume SAW.
***
Katika siku kama ya leo miaka 1155 iliyopita, kilianza kipindi cha vita vya miaka 25 kati ya Uingereza na Denmark katika karne ya 9. Alfred The Great, mfalme kijana wa Uingereza alikuwa kamanda mashuhuri wakati wa kujiri vita hivyo katika kipindi hicho. Wadenmark katika siku hiyo waliivamia Uingereza na kuiteka ardhi kubwa ya nchi hiyo. Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 25 hatimaye vilifikia tamati kwa Waingereza kupata ushindi mnamo tarehe 9 Januari mwaka 896.
***
Miaka 245 iliyopita katika siku kama ya leo William Herschel, mtaalamu maarufu wa nujumu wa Uingereza alifanikiwa kugundua hakika ya kundi la nyota na sayari ikiwemo hii yetu ya dunia. Alitumia darubini kubwa aliyokuwa ametengeneza kwa ajili ya kutazama nyota na kuthibitisha kwamba, kundi la nyota na sayari linaundwa na nyota nyingi ikiwemo sayari ya dunia ambayo ni sehemu ndogo sana ya kundi hilo. Herschel pia ndiye mvumbuzi wa sayari ya Uranus. Alifariki dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 84.
***
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Zuheir Muhsein, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya al Sa’iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa mashirika ya ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) na lile la Misri huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Maajenti wa tawala hizo mbili walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo. Zuheir Muhsin alikuwa mpinzani mkubwa wa mapatano ya kisaliti ya Camp David na aliwahi kutishia mara kadhaa kwamba harakati yake ya al Sa’iqa itamuua mtawala wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadaat aliyetia saini makubaliano hayo na wazayuni.
***
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lilizitaka nchi mbili za Iran na Iraq kusitisha vita na kufanya suluhu. Jamhuri ya Kiislamu ilikubali azimio hilo kutokana na baadhi ya vipengele vyake hususan kile kinachohusiana na kuitambulisha Iraq kuwa ndiye mchokozi katika vita hivyo na kuitaka iilipe Iran fidia ya hasara za vita hivyo. Hata hivyo utawala wa Saddam Hussein ambao pia ulikubali azimio hilo la Baraza la Usalama, uliendeleza mashambulizi dhidi ya ardhi ya Iran.
***
Na tarehe 18 Julai, ni “Siku ya Kimataifa ya Mandela”.
Mwaka wa 2009, Umoja wa Mataifa ulitangaza siku hii kuwa siku mahsusi kwa Nelson Mandela, mwasisi wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Umoja wa Mataifa uliitangaza siku ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, yaani tarehe 18 Julai kuwa Siku ya Kimataifa ili kuenzi mchango wake mkubwa katika harakati ya kupigania uhuru nchini Afrika Kusini na juhudi zake kubwa za kutangaza amani, kutilia maanani utatuzi wa migogoro baina ya kaumu na nchi mbalimbali, kutetea haki za binadamu, na kuwepo usawa na maelewano baina ya wanadamu wa mbari na kaumu zote. Mandela alifariki dunia tarehe 5 Disemba mwaka 2013.