
Afisa mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Mapambano ya Palestina, Hamas, ametoa pongezi za dhati kwa Uhispania kufuatia ushindi wake baada ya mechi ngumu katika fainali ya Kombe la Dunia la FIFA la mwaka 2026, akielezea mafanikio hayo kuwa ni chanzo cha furaha kwa watu wa Palestina na wafuasi wote wa haki, huku akibainisha kuwa ushindi huo ni pigo hasa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na wafadhili wake.
Basem Naim, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, ametoa pongezi kwa timu ya taifa ya Uhispania kwa “ushindi wake wa haki.”
Pia ametuma salamu za pongezi kwa watu wa Palestina na wafuasi wao kote ulimwenguni ambao walisherehekea ushindi huo kwa shauku kubwa.
Naim amesema. “Kama ushindi huu haukuwa na mafanikio mengine isipokuwa kuwakera Wazayuni na mamluki wao, hiyo ingekuwa inatosha.”
Ushindi wa Uhispania umewafurahisha watu kote Palestina na miongoni mwa wafuasi wa mhimili wa Muqawama ulimwenguni kote. Timu ya Uhispania imekuwa ishara ya mshikamano na kadhia ya Palestina, kwa sehemu kubwa kutokana na msimamo wa kisiasa wa kikanuni wa Uhispania dhidi ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel huko Gaza. Aidha Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel alitangaza wazi kuunga mkono timu ya Argentina kutokana na kwa nyote wa timu hiyo Lionel Messi ni mfuasi mkubwa wa Wazayuni
Serikali ya eneo la Madrid nchini Uhispani imetambua Taifa la Palestina, imeweka vikwazo dhidi ya utawala huo vamizi, na kuvunja uhusiano wa kidiplomasia ikiwa ni jibu kwa mauaji na uharibifu unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina.
Aidha nyota wa Uhispania Lamine Yamal, ambaye amekuwa shujaa huko Gaza, aliwahi kupeperusha bendera ya Palestina wakati wa sherehe za ubingwa wa La Liga wa Barcelona, kitendo ambacho kilichochea kuchorwa kwa michoro ya mchezaji huyo kijana katika vitongoji vilivyoharibiwa na vita katika eneo hilo lililozingirwa na Israel.
Aidha msimamo wa Uhispani wa kupinga vita vya kigaidi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran umewavutia wengi duniani kote ambao wameishabikia timu hiyo.
Ushindi wa Uhispania, ingawa ni mafanikio ya michezo, unabeba uzito mkubwa wa kisiasa kwa kuangazia kutengwa kwa utawala wa Kizayuni katika jukwaa la kimataifa na kuchukizwa kwa jamii ya kimataifa na uhalifu wake.
Wakati watu wa Palestina wakiendeleza mapambano yao ya kishujaa, matukio kama haya hutumika kama ukumbusho kwamba kadhia ya haki inavuka mipaka. Furaha iliyopo Palestina na miongoni mwa wafuasi wake kufuatia mafanikio ya Uhispania inasisitiza roho isiyoweza kuvunjika ya taifa linalokataa kufutika, hata linapokabiliwa na mojawapo ya mashambulizi ya kikatili zaidi katika historia ya kisasa.
Uhispania imeibuka bingwa wa Kombe la Dunia baada ya kuichapa Argentina mabao 1-0 katika fainali iliyohitaji muda wa nyongeza, huku Ferran Torres akifunga bao la ushindi lililowavunja nguvu mabingwa watetezi. Fainali hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey, ilimalizika bila mabao ndani ya dakika 90 za kawaida na hivyo kuamuliwa katika muda wa nyongeza.
Katika mchezo huo, Uhispania ilionekana kutawala na kuunda nafasi nyingi zaidi za kufunga, wakati Argentina ilijikita zaidi katika mbinu za kuvuruga kasi ya mchezo na kuchelewesha muda. Mambo yalizidi kuwa magumu kwa Argentina baada ya Enzo Fernandez kuonyeshwa kadi nyekundu muda mfupi kabla ya kuanza kwa muda wa nyongeza.
Dakika ya 106, Ferran Torres aliifungia Hispania bao la ushindi baada ya kupokea mpira wa kichwa uliotolewa na Nico Williams, ambaye alikuwa ameingia akitokea benchi, kisha akampiga mlinda mlango Emiliano Martinez kwa shuti kali la karibu.
Kwa ujumla, fainali hiyo ilikuwa ya ushindani mkubwa, ikipewa uzito zaidi na mapambano ya kimwili na tahadhari za pande zote kuliko soka la kushambulia. Hata hivyo, nje ya uwanja kulikuwa na shamrashamra kubwa, huku mastaa mbalimbali wakihudhuria kushuhudia mechi hiyo ya kihistoria.