Maelfu ya watu walikusanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, kushiriki maandamano ya kuunga mkono serikali na kupinga madai ya kampeni ya mamlaka katika eneo la Tigray kuwasajili kwa lazima vijana kupigana vitani.

Mabango yaliyobebwa na waandamanaji yalikuwa na jumbe mbalimbali kama, “serikali ya Ethiopia lazima itimize wajibu wake wa kuwalinda watu wa Tigray” na pia “sitisheni kuwasafirisha wapiganaji kwenda Sudan!”

Serikali ya Ethiopia pamoja na baadhi ya vyombo vya habari vya nchi hiyo, zimeishutumu TPLF kwa kuwalazimisha raia wa Tigray kwenda Sudan. Hata hivyo, hakuna ushahidi uliotolewa kuunga mkono madai hayo.

Shirika la kutetea hazi za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetangaza kuwa, mamlaka za kikanda katika eneo la kaskazini mwa Tigray nchini Ethiopia zimekuwa zikiwateka nyara na kuwaajiri raia kinyume cha sheria hasa watoto wenye umri wa miaka 15, tangu Aprili 2026.

Katika taarifa iliyotolewa 6 Julai 2026, shirika hilo lilisema kwamba, jamii katika miji na vijiji zinasema vikosi vya jeshi na maafisa wa Tigray wanawakamata wapiganaji wa zamani, wanaume na wavulana kutoka mitaani, ofisini, majumbani wakati wa upekuzi wa usiku, na maeneo ya kuchimba dhahabu.

“Kampeni ya mamlaka ya Tigray ya kuwaajiri wanaume na wavulana kwa nguvu katika vikosi vyao inazusha hali ya hofu katika eneo lote,” anasema Laetitia Bader, naibu mkurugenzi wa Afrika wa HRW.

Human Rights Watch imesajili visa sita vya kulazimishwa kuajiriwa kupitia mahojiano ya mbali na watu 18 mwezi Juni, wakiwemo mashahidi, jamaa za wapiganaji walioandikishwa jeshini, na wale waliotoroka baada ya kutekwa nyara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *