
Gazeti la Eurasia Daily limeripoti kuwa mvutano unaoendelea katika eneo la Asia Magharibi umesababisha akiba ya mafuta ya Marekani kushuka hadi kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 43 iliyopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali ya sintofahamu ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Mashariki ya Kati imeathiri masoko ya nishati, huku Marekani ikikabiliwa na upungufu mkubwa katika hifadhi zake za mafuta.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, kupungua akiba hiyo kunaonyesha athari za moja kwa moja za mivutano ya kikanda kwenye usalama wa nishati wa Marekani na masoko ya kimataifa ya mafuta.
Gazeti la Eurasia Daily limeripoti kuhusu kupungua akiba ya kimkakati ya mafuta ya Marekani, likisema kuwa, kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Habari za Nishati ya Marekani, hifadhi hiyo imeshuka hadi mapipa milioni 319.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa kiwango hicho ndicho cha chini zaidi kuwahi kufikiwa na akiba ya kimkakati ya mafuta ya Marekani katika kipindi cha miaka 43 iliyopita, tangu mwaka 1983.
Aidha, gazeti hilo limebainisha kuwa kiwango hicho ni pungufu kwa mapipa milioni 27 ikilinganishwa na kiwango cha chini kabisa cha akiba hiyo kilichorekodiwa wakati wa utawala wa Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden.
Katika mkutano wa mwezi Machi 2026 wa nchi wanachama wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), Marekani ilijitolea kutoa sehemu ya akiba yake ya kimkakati ya mafuta, inayojulikana kama Strategic Petroleum Reserve (SPR).
Hatua hiyo ililenga kusaidia kudhibiti hali ya soko la nishati na kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mafuta katika kipindi cha mvutano wa kikanda na mabadiliko katika usambazaji wa nishati duniani.
Akiba ya kimkakati ya mafuta ya Marekani ni hifadhi kubwa ya dharura inayotumiwa na serikali wakati wa changamoto kubwa za kiusalama, kiuchumi au misukosuko katika soko la mafuta duniani.