
Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua mpya katika safari ya kuelekea matumizi ya usafiri wa umeme baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutoa mwongozo maalumu wa vituo vya kuchajia magari ya umeme na mifumo ya kubadilisha betri.
Mwongozo huo unafungua ukurasa mpya kwa wawekezaji na watumiaji wa teknolojia hiyo huku ukiweka misingi ya usalama, uwekezaji na uendeshaji wa miundombinu inayohitajika kuendesha sekta ya magari ya umeme nchini.
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea kuchochea ajenda ya nishati safi na uchumi wa kijani, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa.
Kwa miaka kadhaa, matumizi ya magari ya umeme nchini yalikuwa yanakabiliwa na changamoto za miundombinu, ukosefu wa mwongozo mahsusi na kutokuwepo kwa viwango vya pamoja vya kiufundi kwa waendeshaji wa huduma hizo.
Sasa, kupitia mwongozo huo, Ewura imeweka masharti yanayolenga kuhakikisha vituo vya kuchajia vinajengwa kwa viwango vinavyokubalika huku usalama wa watumiaji na miundombinu ya umeme ukipewa kipaumbele.
Mtazamo wa wachumi
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude, anasema hatua hiyo ilikuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu kutokana na ongezeko la magari na pikipiki za umeme pamoja na hitaji la kuwa na mfumo rasmi wa usimamizi.
Anasema kwa muda mrefu mifumo mingi ya usajili na utambuzi wa vyombo vya moto ilikuwa imejengwa kwa kuzingatia magari yanayotumia mafuta, jambo lililosababisha changamoto kwa teknolojia mpya za umeme.
Kwa mujibu wake, baadhi ya waingizaji wa pikipiki za umeme walikumbana na ugumu wa usajili kutokana na kukosekana kwa utaratibu maalumu wa kuzitambua katika mifumo iliyokuwapo.
“Kwa muda mrefu mifumo yetu ilizoea kutambua magari ya mafuta. Hata pikipiki za umeme zilikuwa zinakabiliwa na changamoto za kiutambuzi kwa sababu hakukuwa na mfumo mahsusi wa kuzisimamia,” anasema.
Mkude anasema mwongozo huo pia utasaidia kudhibiti matumizi holela ya miundombinu ya kawaida ya nyumbani kuchajia magari yenye matumizi makubwa ya umeme.
Anasema mahitaji ya umeme kwa gari ni tofauti na yale ya vifaa vya kawaida vya nyumbani, hivyo uwepo wa viwango vya kitaalamu utasaidia kupunguza hatari za hitilafu na ajali.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kijamii, Magabilo Masambu, anasema mwongozo huo umeweka msingi muhimu wa maendeleo ya sekta ya usafiri wa umeme kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Anasema uwekezaji katika teknolojia mpya huhitaji uhakika wa kisheria na kiutendaji, jambo ambalo sasa limeanza kupatikana kupitia mwongozo huo wa Ewura.
Kwa mujibu wake, wawekezaji wanahitaji kujua wajibu wao, taratibu za kufuata na masharti ya usalama kabla ya kuwekeza fedha nyingi katika miundombinu ya kuchajia magari ya umeme.
“Hatua hii itaongeza imani kwa wawekezaji, kupunguza changamoto za kiufundi na kusaidia kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kijani unaotegemea matumizi ya nishati safi,” anasema.
Masambu, anasema nchi nyingi duniani zimefanikiwa kukuza matumizi ya magari ya umeme kwa kuanza kuweka mifumo madhubuti ya udhibiti kabla ya ongezeko kubwa la watumiaji.
Anaeleza kuwa Tanzania ina nafasi ya kujifunza kutoka kwa mataifa hayo kwa kujenga mazingira rafiki yatakayowezesha sekta hiyo kukua kwa kasi na kwa usalama.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, wawekezaji watakaotaka kuanzisha vituo vya kuchajia vinavyotoa huduma kwa umma watalazimika kuomba kuunganishiwa umeme kupitia kampuni husika za usambazaji wa umeme.
Mahitaji ya umeme yatakapoonekana kuwa makubwa, waendeshaji wanaweza kutakiwa kufunga transfoma maalumu pamoja na kuboresha miundombinu ya usambazaji wa umeme katika maeneo husika.
Pia watahitajika kufunga mifumo ya kinga inayozingatia kanuni za usambazaji wa umeme nchini ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa usalama na ufanisi unaokubalika.
Wawekezaji watawajibika kupata maeneo yanayofaa kwa ajili ya vituo hivyo pamoja na vibali vya ujenzi kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Ewura imeweka msisitizo mkubwa katika masuala ya usalama kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa kuchajia magari yenye matumizi makubwa ya nishati.
Waendeshaji wa vituo watatakiwa kuwa na vifaa vya kuzimia moto vinavyokidhi viwango vinavyotakiwa na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa nyaya na mashine za kuchajia.
Maelekezo ya mwongozo
Mwongozo huo pia unataka magari yenye hitilafu za mfumo wa umeme yasichajiwe hadi yatakapofanyiwa matengenezo ili kupunguza uwezekano wa ajali.
Aidha, inapendekezwa kuwepo kwa mfumo wa kuzima umeme moja kwa moja pindi joto litakapozidi kiwango kinachokubalika ili kuzuia madhara makubwa.
Katika upande wa miundombinu, Ewura imeweka mapendekezo ya ukubwa wa maeneo yatakayotumika kujenga vituo vya kuchajia magari ya umeme.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, kituo kidogo chenye vifaa viwili vya kuchajia kinashauriwa kuwa na eneo la kati ya mita za mraba 40 na 60.
Kwa vituo vikubwa vinavyotoa huduma ya kuchajia kwa kasi, eneo linalopendekezwa ni kati ya mita za mraba 300 na 600 kutegemea ukubwa wa huduma.
Vituo hivyo vinatakiwa kuwa na huduma muhimu ikiwemo maji, taa, vyoo, kamera za ulinzi, walinzi na maeneo salama ya kuingia na kutoka magari.
Mwongozo huo pia umefungua fursa ya matumizi ya mifumo ya nishati ya jua na betri za kuhifadhi umeme katika vituo vya kuchajia.
Hata hivyo, mifumo hiyo italazimika kuzingatia viwango vya kitaifa vya usalama pamoja na masharti ya kuunganishwa kwenye gridi ya taifa.
Katika hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma, Ewura imependekeza vituo vya kuchajia vijengwe kwa umbali usiozidi kilomita 50 katika barabara kuu.
Mapendekezo hayo pia yanahusu maeneo ya mijini ambapo matumizi ya magari ya umeme yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Kwa magari makubwa yanayosafiri masafa marefu, mwongozo unapendekeza kuwepo kwa angalau kituo kimoja cha kuchajia kwa kasi kila baada ya kilomita 100.
Hatua hiyo inalenga kupunguza hofu ya watumiaji kuhusu upatikanaji wa huduma za kuchajia wanapokuwa safarini katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, vituo vya mafuta vitaruhusiwa kufunga vifaa vya kuchajia magari ya umeme kwa kuzingatia masharti yote ya usalama yaliyowekwa.
Wataalamu wanaamini hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma kwa sababu vituo vya mafuta tayari vina mtandao mpana wa huduma katika maeneo mengi.
Waendeshaji wa vituo watahitajika kuwasilisha taarifa kwa Ewura kila baada ya miezi sita kuhusu shughuli zao za uendeshaji.
Taarifa hizo zitajumuisha maeneo ya vituo, aina za vifaa vya kuchajia, uwezo wa huduma, saa za kazi na gharama zinazotozwa kwa wateja.
Kwa upande wa Serikali, lengo lililowekwa ni kuhakikisha asilimia 20 ya vyombo vya moto vinavyoingia nchini vinatumia umeme katika miaka ijayo.
Akizungumza Juni 11, 2026 wakati wa uzinduzi wa kituo cha kuchajia magari ya umeme Dodoma, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisisitiza umuhimu wa teknolojia hiyo.
Alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kufikia malengo hayo kutokana na ongezeko la matumizi ya magari na pikipiki za umeme katika maeneo mbalimbali.
Alifafanua moja ya faida kubwa za magari ya umeme ni gharama ndogo za uendeshaji ikilinganishwa na magari yanayotumia mafuta.
Alisema safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma inaweza kugharimu kati ya Sh250,000 na Sh300,000 kwa gari la mafuta.
Kwa upande wa gari la umeme, kiwango hicho cha safari kinaweza kuhitaji umeme wa thamani ya kati ya Sh27,000 na Sh28,000 pekee.
Tofauti hiyo ya gharama inaendelea kuvutia wananchi wengi na wafanyabiashara kuanza kuangalia uwezekano wa kuhamia katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Ripoti ya mwaka 2023 ya Africa E-Mobility Alliance inaonyesha uwekezaji katika sekta ya usafiri wa umeme nchini unaendelea kuongezeka kwa kasi.
Pikipiki na bajaji za umeme zimeendelea kuongoza ukuaji huo kutokana na gharama nafuu za matumizi, urahisi wa matengenezo na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme.