Chanzo cha picha, Reuters
Jaji wa Marekani ameamua kuwa Ismael “El Mayo” Zambada, mmoja wa watu mashuhuri na hatari zaidi katika magenge ya dawa za kulevya nchini Mexico, atatumikia kifungo cha maisha gerezani; uamuzi huu umetolewa miaka miwili baada ya kiongozi huyo mkuu kushawishiwa kuja Marekani kupitia operesheni maalum na ya siri iliyopangwa kwa ustadi.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 76, ambaye alianzisha Genge la Sinaloa (Sinaloa Cartel) pamoja na Joaquin “El Chapo” Guzmán, aliomba radhi mahakamani na pia akaamriwa kulipa dola bilioni 15 (pauni bilioni 11).
Mnamo mwaka wa 2024, mtoto wa El Chapo alimshawishi Zambada kuamini kuwa walikuwa wakisafiri kwenda kaskazini mwa Mexico kukagua viwanja vya ndege vya siri, lakini badala yake ndege yao ilitua Texas ambapo alikamatwa.
Mwaka jana, Zambada alifikia makubaliano na upande wa mashtaka na kukiri makosa ya kusafirisha dawa za kulevya na kula njama, ili kuepuka adhabu ya kifo. Siku ya Jumatatu, Jaji wa Wilaya ya Marekani Brian Cogan alitoa hukumu dhidi ya Zambada katika kikao cha mahakama ya shirikisho huko Brooklyn.
Kukiri kwake hatia kulileta adhabu ya lazima ya kifungo cha maisha gerezani. Zambada alizungumza kupitia mkalimani wa lugha ya Kihispania wakati wa kikao hicho. Alisema anaomba radhi “kwa madhara niliyosababisha na kwa mfano mbaya nilioonyesha” na akatoa wito kwa vizazi vijavyo “kuchagua njia tofauti”.
“Kama kuna jambo moja ninaloweza kusema lenye thamani leo, ni hili: ni lazima vurugu na uhalifu wa kikatili vikome,” alisema kiongozi huyo wa zamani wa genge la dawa za kulevya.