Jeshi la Israel jana lilifanya operesheni kubwa ya ubomoaji kusini mwa Lebanon siku ya Jumatatu huku ndege zisizo na rubani za utawala huo ghasibu zikiruka katika anga ya mji mkuu wa chi hiyo Beirut na vitongoji vyake.

Vyombo vya habari vya Lebanon vimearifu kuwa hujuma hiyo ya Israel ni katika ukiukaji mpya wa kalibu ya makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani.

Shirika la Habari la Taifa la Lebanon (NNA) linaloendeshwa na serikali limeripoti kuwa mlipuko mkubwa ulisikika kabla ya saa sita mchana jana Jumatatu, na baadaye ikathibitishwa kuwa ulisababishwa na operesheni ya Israel ya kubomoa majengo katika mji wa kusini wa Kfartebnit. Mawingu mazito ya moshi yalionekana yakipanda juu katika eneo hilo.

Wakati huo huo, katika wilaya ya kusini ya Marjayoun milipuko mitatu mfululizo ilisikika huko Qlayaa. Shirika la Habari la Taifa la Lebabon lilitangaza kuwa milipuko hiyo ilisababishwa na ulipuaji wa kudhibitiwa uliofanywa na jeshi la Lebanon ili kuteketeza mada za milipuko ambazo hazikuwa zimelipuka, makombora na roketi yaliyotelekezwa katika mapigano ya awali.

Kwingineko, Shirika la Habari la Lebabon jana lilitangaza kuwa ndege isiyo na rubani ya Israel ilidondosha guruneti la kushtua (stun grenade) katika mji wa Mansouri, eneo la Tyre kusini mwa Lebanon.

Kwa mujibu wa shirika hilo, ndege zisizo na rubani za Israel pia zilishuhudiwa zikiruka katika anga ya Beirut na vitongoji vyake, huku ndege za kivita za Israel zikifanya mazoezi ya mashambulizi kando ya mpaka wa kaskazini wa Lebanon na juu ya maeneo yenye milima ya Akkar kaskazini na Hermel mashariki.

Hujuma hizo za Israel zimeripotiwa huku jeshi la utawala huo likiendeleza mashambulizi dhidi ya Lebanon, licha ya makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Beirut na Tel Aviv chini ya upatanishi wa Marekani mwezi uliopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *