RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za pole kwa Amir wa Qatar, Serikali na wananchi wa taifa hilo kufuatia kifo cha Amir wa zamani wa Qatar, Hayati Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani.
Rais Dk. Mwinyi ametoa salamu hizo leo, Julai 21, 2026, alipofika katika Ubalozi wa Qatar nchini Tanzania, uliopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam, ambako alisaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha kiongozi huyo. SOMA: Dk Mwinyi aanika mafanikio lukuki afya, amani, Muungano

Akiwa ubalozini hapo, Rais Dk. Mwinyi, kupitia kwa Balozi wa Qatar nchini Tanzania Fahad Rashid Al-Muraikhi, alituma salamu za pole kwa Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, familia ya kifalme, Serikali na wananchi wa Qatar kutokana na msiba huo mkubwa.
Amesema Hayati Sheikh Hamad ataendelea kukumbukwa kwa uongozi wake wenye maono, mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Qatar, pamoja na juhudi zake za kuimarisha elimu, uchumi, ustawi wa wananchi na nafasi ya taifa hilo katika masuala ya kimataifa. Hayati Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani alifariki dunia Julai 12, 2026, akiwa na umri wa miaka 74.