
Msemaji wa Jeshi la Yemen ametangaza marufuku ya usafiri wa meli na kuweka mzingiro wa majini dhidi ya Saudi Arabia, kwa kuzingatia kanuni ya “mzingiro kwa mzingiro.”
Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen, alitoa taarifa tarehe 20 Julai akitangaza mzingiro huo wa majini dhidi ya Saudi Arabia. Alibainisha kuwa kwa takriban miaka 12, Saudi Arabia imekuwa ikishambulia bandari na viwanja vya ndege vya Yemen kupitia mizingiro ya nchi kavu, baharini na angani, jambo ambalo limeendelea kuwatesa wananchi wa Yemen, kupelekea kuporwa rasilimali zao na kuongeza mashinikizo dhidi yao.
Taarifa hiyo imesema mzingiro dhidi ya Yemen hauna msingi wowote wa kisheria au kibinadamu, na kusisitiza kuwa watu wa nchi hiyo wana haki ya kujibu hatua hii na mashambulizi ya Saudia, ikiwa ni pamoja na mzingiro wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana’a, kwa kutumia mbinu zote zilizopo. Imesisitiza zaidi juu ya haki ya watu wa Yemen ya kukabiliana na mzingiro kwa mzingiro na pia kujibu ongezeko lolote la uadui kwa ongezeko sawa la ulipizaji kisasi na la pande zote.
Mohammed Abdulsalam, Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya Yemen, awali alisisitiza kwamba, tangazo la mzingiro wa jeshi la majini dhidi ya Saudi Arabia na wanajeshi wa Yemen ni hatua ambayo Sana’a imelazimika kuichukua ili kujibu hatua ya Riyadh ya kukataa kujibu matakwa halali ya watu wa Yemen kwa njia ya amani. Saudi Arabia imelaani tangazo la jeshi la Yemen la kuweka mzingiro wa majini dhidi yake. Kupitia taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imetangaza kuwa Riyadh itachukua hatua zote zinazohitajika kwa ajili ya kulinda meli zake kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Baada ya kuvumilia kwa miaka mingi mzingiro uliowekwa na utawala wa Saudi Arabia, ukiungwa mkono na nchi za Magharibi, hatimaye Wayemen wametangaza mlinganyo mpya wa “mzingiro kwa mzingiro” katika makabiliano yao na Saudia. Hatua hii ya Yemen kulipiza kisasi imekuwa ikitarajiwa kwa muda mrefu katika ngazi ya kikanda.
Riyadh inachukulia tishio hili kwa uzito mkubwa, ikiamini kuwa Sana’a ina uwezo wa kijeshi wa kufunga njia muhimu ya majini ya Babul Mandab, njia ambayo umuhimu wake katika biashara ya kimataifa umeongezeka zaidi kutokana na mivutano ya kijiopolitiki inayoendelea katika Lango-Bahari la Hormuz.
Kubana matumizi ya Lango-Bahari la Bab al-Mandab kama mbinu ya kutoa mashinikizo, mkakati mpya unaotumiwa na Ansarullah ya Yemen kwa ajili ya kuzuia uchokozi wa Saudi Arabia, umeanza kutekelezwa hivi karibuni. Chini ya mkakati huu, iwapo Saudi Arabia itakataa kutekeleza matakwa ya Wayemen, chaguo la “vita kamili” dhidi ya Riyadh litawekwa mezani.
Katika muktadha huu, na kwa mara ya kwanza tangu vita vya Yemen vianze mwezi Machi 2015, kumekuwa na mjadala kuhusu uwezekano wa kuzuia meli za mafuta za Saudi Arabia kupita katika lango hilo. Wataalamu wa masuala ya uchumi wanaamini kuwa hali hiyo inaweza kupelekea bei ya mafuta kupanda na kuvuka dola 150 kwa pipa, kwani inaweza kuvuruga usafirishaji wa kila siku wa mapipa zaidi ya milioni 7 ya mafuta ya Saudia, ambayo husafirishwa kupitia Bomba la Mafuta la Mashariki-Magharibi hadi bandari ya Yanbu, na hivyo kuathiri moja kwa moja mapato ya nchi hiyo yanayotokana na mafuta. Mbali na hayo, kusitishwa usafirishaji wa mafuta, hata kwa siku chache tu, kunaweza kuzidisha mgogoro wa upatikanaji wa nishati na kupelekea kuyumba kwa kiasi kikubwa soko la mafuta duniani, hasa wakati ambapo bei ya mafuta kimataifa tayari imepanda kutokana na kufungwa Lango Bahari la Hormuz kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran. Madhara ya mvutano huu hayataishia kwenye bandari ya Yanbu pekee; bandari ya Jeddah, ambayo hivi karibuni imeibuka kama kitovu muhimu cha usafirishaji na njia mbadala ya Lango la Hormuz, pia itakabiliwa na usumbufu. Ikizingatiwa kuwa takriban asilimia 70 ya bidhaa zinazoingizwa nchini Saudi Arabia hupitia Jeddah, na kwamba bandari hiyo ina nafasi muhimu katika usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi za Ghuba ya Uajemi kama vile Qatar, Kuwait, na Bahrain, hivyo kusimama kwa shughuli zake kunaweza kuibua mgogoro mkubwa katika mifumo ya usambazaji, sekta za uzalishaji na mazingira ya uwekezaji katika eneo.
Chini ya kanuni ya ulipizaji kisasi ya “bandari-kwa-bandari”, bandari za Yanbu na Jeddah ni miongoni mwa bandari muhimu zinazoweza kushambuliwa ikiwa Saudia itaendelea kuizingira Yemen au kudumisha muungano wa kijeshi unaoongozwa na nchi hiyo dhidi ya Sana’a.
Kwa hivyo, inaonekana kwamba vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen si tena makabiliano ya kijeshi kwenye mipaka ya mataifa hayo mawili, bali vimebadilika na kuwa mzozo unaohusisha mienendo ya usalama wa nishati ya kikanda na njia za kimkakati. Wakati Yemen ikitangaza uwezo mpya wa kuzuia uchokozi wa maadui ili kukabiliana na mzingiro unaoendelea wa Saudi Arabia, ongezeko lolote la mvutano katika Bahari Nyekundu na Lango-Bahari la Bab al-Mandab linaweza kuathiri biashara ya kimataifa, masoko ya nishati na usalama wa baharini, taathira ambazo zinavuka mipaka ya Saudi Arabia yenyewe. Hivyo, tishio lililotolewa na Yemen, hasa lile la kuweka mzingiro wa majini dhidi ya Saudi Arabia, si sehemu ya vita vya vyombo vya habari; bali linaashiria mabadiliko halisi katika uwiano wa nguvu yaliyojitokeza katika miaka ya vita na mzingiro uliowekwa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, mabadiliko ambayo sasa yanaweza kuwalazimu wadau wa ndani na nje ya eneo kutathmini upya mikakati na mahesabu yao.