Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Amir Hatami, ametoa onyo kali kwamba uvamizi wowote wa nchi kavu wa jeshi la Marekani utakabiliwa na jibu la kijeshi la kuangamiza. Amesisitiza kuwa mamilioni ya Wairani wako tayari kuwakabili wavamizi kwa kila nyenzo waliyo nayo, huku Majeshi ya Ulinzi yakiwa katika utayari wa hali ya juu dhidi ya uchokozi wowote.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika vitengo mbalimbali vya Jeshi la Nchi Kavu, Kikosi cha Ulinzi wa Anga, na Jeshi la Anga katika mkoa wa Isfahan siku ya Jumatano, Jenerali Hatami amesema kuwa tawala adui zimefanya kila hila dhidi ya askari wa Iran, lakini zimeshindwa kulegeza azma yao ya kulinda nchi.

Akirejelea matarajio ya Marekani wakati wa operesheni zao zilizofeli kusini mwa Isfahan, Jenerali Hatami amesema Washington imefanya makosa makubwa ya kimahesabu.

Jenerali Hatami amesisitiza kuwa Iran haijawahi kuamini maadui zake katika kuheshimu ahadi zao za makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo, na hivyo huchukua hatua za kuendelea kuimarisha utayari wake wa kijeshi.

Aidha kamanda huyo ameonyesha imani yake katika ustahimilivu wa taifa la Iran, na kusema: “Taifa la Iran ni taifa lenye heshima kubwa duniani.”

Akiangazia msimamo wa kijeshi wa Iran katika eneo la Asia Magharibi, kamanda huyo amesema kuwa nchi imesimama kidete dhidi ya mataifa makubwa ya kijeshi duniani katika kipindi cha vita viwili vya hivi karibuni. Mkuu huyo wa Jeshi pia amebainisha kuwa wengi walitarajia Iran idhalilishwe, lakini malengo hayo yamefeli.

Kauli hizi zinakuja kufuatia raundi mbili za uchokozi wa kijeshi uliofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran katika mwaka uliopita. Iran ilijibu kwa kutekeleza operesheni pana za makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani (drones) dhidi ya ngome za kijeshi za Israel na Marekani katika eneo la Asia Magharibi, hatua iliyoonyesha uwezo unaokua wa kuzuia mashambulizi wa nchi hii na utayari wake wa kujibu kwa dhati uchokozi wowote wa baadaye.

Iran imesisitiza mara kwa mara kuwa itikadi yake ya kijeshi ni ya kujilinda  na kwamba uwezo wake wa makombora na ndege zisizo na rubani unalenga kuzuia mashambulizi na kulinda uhuru na utimilifu wa ardhi ya nchi.

Maafisa wa Iran wameendelea kuonya kuwa ukiukaji wowote wa mamlaka ya nchi hii utakabiliwa na jibu la haraka na lenye nguvu linalolenga ngome za kijeshi na maslahi ya kimkakati ya wavamizi katika kanda nzima.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *