ARUSHA: Wagonjwa 258 waliobainika kuhitaji upasuaji mkubwa katika Kambi ya Matibabu ya Bure iliyoratibiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, wanatarajiwa kuanza kupatiwa matibabu ya kibingwa wiki ijayo katika hospitali mbalimbali za rufaa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Makonda alisema wagonjwa hao watapelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, Kituo cha Tiba cha KCMC mkoani Kilimanjaro, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kulingana na aina ya matibabu wanayohitaji.

Alisema wagonjwa 172 kati ya hao watafanyiwa upasuaji katika hospitali za jijini Arusha, huku zoezi hilo likisimamiwa na Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha, Dk. Nindwa Maduhu.

Aidha, wagonjwa wengine 86 watasafirishwa kwenda Moshi na Dar es Salaam kwa ajili ya upasuaji maalumu unaohusisha magonjwa ya moyo, uti wa mgongo pamoja na uvimbe wa ubongo, ambao unahitaji huduma za kibingwa zaidi.

Makonda alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa mafanikio ya kambi ya matibabu ya siku nane iliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambapo jumla ya wananchi 24,871 walipata huduma mbalimbali za afya bila malipo.

Alibainisha kuwa huduma hizo hazikuwahusu wakazi wa Arusha pekee, bali zilinufaisha wananchi kutoka mikoa saba tofauti, kwani kambi hiyo ilikuwa wazi kwa Watanzania wote waliokuwa na uhitaji wa matibabu.

Kwa mujibu wa Makonda, wagonjwa 230 walifanyiwa upasuaji moja kwa moja ndani ya kambi hiyo kupitia huduma zilizotolewa na madaktari bingwa na wabobezi kutoka hospitali za serikali na binafsi.

Alisema jumla ya wahudumu wa afya 720, wakiwemo madaktari bingwa, wauguzi na wataalamu wengine, walishiriki kutoa huduma katika kambi hiyo.

Makonda pia alisema kati ya fedha zilizochangwa na wadau kwa ajili ya kufanikisha kambi hiyo, kiasi cha shilingi milioni 174 kimebakia, sambamba na dawa, vifaa tiba na vifaa vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 89.8.

Aliwashukuru wadau wote waliochangia kufanikisha zoezi hilo, wakiwemo taasisi za umma na binafsi, kampuni za dawa, maduka ya dawa, marafiki na wananchi mbalimbali, akisema ushirikiano wao umewezesha kutoa huduma kwa maelfu ya wagonjwa na kuweka historia ya utoaji wa matibabu ya bure nchini.

Makonda alisema kambi hiyo ilikuwa ya tatu kuandaliwa chini ya uratibu wake, akieleza kuwa alianza utaratibu huo alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, akaendeleza akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na sasa akiwa Waziri na Mbunge wa Arusha Mjini.

Aliongeza kuwa maandalizi ya kambi ya mwaka ujao tayari yameanza, huku madaktari bingwa kutoka Hispania na Ujerumani wakithibitisha kushiriki, akiwemo daktari bingwa wa macho anayefahamika kimataifa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Charles Mkombachepa, alimpongeza Makonda kwa kuwaamini wataalamu wa afya kuendesha shughuli zote za kambi bila kuingiliwa.

Alisema uhuru huo uliwawezesha kufanya kazi kwa weledi na kujituma, jambo lililochangia mafanikio makubwa ya kambi hiyo na kuwafanya wananchi wengi kupata huduma za matibabu kwa wakati.

Dk. Mkombachepa alieleza kuwa hatua hiyo inastahili pongezi kwa kuwa imeleta manufaa makubwa kwa wakazi wa Arusha na Watanzania kutoka maeneo mbalimbali waliofika kupata huduma za afya bila malipo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *