RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amezindua  huduma za usafiri wa umma kwa kutumia mabasi ya umeme pamoja na Kituo cha Mabasi cha Malindi, ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa usafiri na kuhamasisha matumizi ya nishati safi visiwani Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Zanzibar Social Security Fund (ZSSF) kuharakisha ujenzi wa vituo vya kisasa vya mabasi ili wananchi waweze kunufaika kikamilifu na huduma hiyo. Amesema mradi wa mabasi ya umeme utachangia kuboresha usafiri wa umma, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuimarisha matumizi ya nishati mbadala. SOMA: Rais Mwinyi awakaribisha Sweden kuwekeza Zanzibar

Aidha, Rais amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, upatikanaji wa maji safi, maendeleo ya bandari, viwanja vya ndege, hospitali pamoja na Mji wa Michezo unaojiandaa kuhudumia mashindano ya AFCON. Vilevile, amewahimiza wananchi kuilinda miundombinu ya umma na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza maendeleo ya taifa.

Hafla hiyo pia ilishuhudia uzinduzi wa kadi maalumu za usafiri kwa wanafunzi, wazee na makundi mengine ya abiria, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri wa umma na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *