
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, amezionya nchi za Ulaya kwamba kutoa kambi au maeneo ya kijeshi kwa Marekani kutaziweka “katika safu ya wavamizi.”
Gharibabadi ametoa onyo hilo kali katika ujumbe uliotumwa kwenye akaunti yake ya X jana Alhamisi baada ya kukutana na wawakilishi na mabalozi 25 wa nchi za Ulaya mjini Tehran.
Ameeleza misimamo ya Iran kuhusu yanayojiri sasa na vitendo vya “kihalifu” vya Marekani na kusema kwamba Iran ilitoa kipigo kikali kwa wavamizi wakati wa vita vya siku 40 vilivyoanzishwa na Marekani na Israel.
“Katika awamu mpya ya uvamizi huo wa kijeshi, tutatetea kwa dhati ardhi yetu na maslahi ya kitaifa,” amesisitiza mwanadiplomasia huyo wa Iran.
Gharibabadi amesema kwamba vita vya sasa havina “mafanikio yoyote ya kimkakati” kwa Marekani, akiongeza kwamba “vinahatarisha amani na usalama wa kikanda na kimataifa.”
Ameongeza: Hata hivyo, miongoni mwa Wazungu wa Ulaya, kuna idadi ndogo ya nchi, ikiwa ni pamoja na Uhispania, ambazo zimeamua kuchukua “misimamo ya kisheria.”
“Hata hivyo, serikali za nchi za Ulaya zinapaswa kujua kwamba kutoa kambi na maeneo yao kwa wavamizi kutaziweka miongoni mwa wavamizi,” amesema Kazem Gharibabadi.
Matamshi yake yamekuja baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham kuidhinisha Marekani kuendelea kutumia kambi za kijeshi za nchi hiyo kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Iran, na kuendeleza sera iliyoanzishwa chini ya mtangulizi wake, Keir Starmer.
Bunge la Bulgaria pia Jumanne iliyopita liliunga mkono pendekezo la serikali la kuruhusu jeshi la Marekani kupeleka ndege za kijeshi katika Kituo cha Anga cha Bezmer ili kuunga mkono mashambulizi na vita dhidi ya Iran.
Akizungumzia hatua hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismael Baqaei amesema Bulgaria inajua vyema kwamba mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran ni ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.