Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Nchi nane za Kiarabu na Kiislamu zimelaani vikali kuingia kwa waziri wa Israel na walowezi katika Msikiti wa Al-Aqsa kupitia taarifa ya pamoja.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Misri, Qatar, Uturuki, Pakistan, na Indonesia walitoa taarifa ya pamoja wakilaani vikali kitendo cha Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, na walowezi wa Israel kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa.
Taarifa hiyo, iliyotolewa jioni ya Alhamisi, Agosti 2, ilieleza kuwa kitendo hiki ni ukiukaji wa wazi wa hali ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa na uchokozi usiokubalika ambao unaweza kusababisha kuongezeka kwa mivutano katika eneo hilo.
Nchi hizo nane pia zilisisitiza yafuatayo:
Haja ya kuheshimu mamlaka ya usimamizi ya Jordan juu ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo mjini Jerusalem;
Kupinga jaribio lolote la kubadilisha hadhi ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa;
Haja ya kusitisha vitendo vya uchokozi na vya upande mmoja ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama na utulivu wa eneo hilo;
Kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Jerusalem. Taarifa hiyo ilitolewa baada ya Itamar Ben-Gvir kuingia katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa akiwa na mamia ya walowezi wa Israel, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali na Wapalestina, Jordan, pamoja na nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu.