Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa, Francesca Albanese, amelaani vikali wimbi kubwa la ghasia zinazotekelezwa na walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika maeneo yote ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel.

Ameihimiza jamii ya kimataifa kuwalinda raia wa Palestina na kuwajibisha utawala wa Israel kwa jinai zilizotendwa dhidi ya ubinadamu.

Albanese ametoa onyo hilo siku ya Ijumaa, akisema kuwa mashambulizi ya kikatili yameripotiwa kote katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, hasa katika eneo la kaskazini na maeneo ya jirani na Nablus.

Ameandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X: “Tahadhari! Mashambulizi ya kikatili yanaripotiwa katika maeneo yote ya Ukingo wa Magharibi, hasa eneo la kaskazini na Nablus!” Ameonya kuwa walowezi wa Kizayuni, wakisaidiwa na vikosi vamizi vya Israel, wanatekeleza mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya Wapalestina.

Amesema kuwa “makundi ya walowezi ambao ni magaidi wakiwa na nguvu zao zote na kuungwa mkono na wanajeshi wa Israel” wanatoa wito wa wazi wa “kumwaga damu.”

Onyo lake limekuja saa chache baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Palestina kutoa wito wa kuingiliwa kati kwa dharura na jamii ya kimataifa ili kusitisha mashambulizi ya magenge ya walowezi wa Kizayuni na vikosi vya uvamizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Wito huo ulifuatia shambulio lililofanywa na walowezi wa Kizayuni wakisaidiwa na wanajeshi wa Israel katika mji wa Tell karibu na Nablus, ambalo lilisababisha vifo vya Wapalestina wanne, kwa mujibu wa mamlaka za Palestina.

Mapema siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu na waziri wa vita wa utawala huo, Israel Katz waliamuru “operesheni kubwa ya kijeshi” inayolenga miji na vijiji vya Palestina kote katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Baadaye, walowezi wa Kizayuni walishambulia vijiji vya Palestina vya Sarra na Urif katika mkoa wa Nablus, wakichoma moto nyumba na mali nyinginezo.

Wakati huo huo Wapalestina sita wameuawa na wengine 37 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel kote Gaza katika saa 48 zilizopita. Hayo ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza

Idadi ya vifo kutokana na uvamizi wa kijeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza imefikia 73,317, wizara hiyo ilisema siku ya Jumamosi, huku mashambulizi ya Israel katika eneo hilo yakiendelea.

Wizara imeongeza kuwa tangu usitishaji mapigano ulipotangazwa Oktoba 10, 2025, Wapalestina 1,191 wameuawa na wengine 3,853 kujeruhiwa.

Pia imesema kuwa maiti za waathiriwa 803 zimeondolewa kutoka chini ya vifusi katika kipindi hicho hicho. Harakati ya muqawama ya Palestina, Hamas, imeilaani vikali Israel kwa kuendelea na vita vyake vya kimbari dhidi ya raia huko Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *