DAR ES SALAAM: SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuhakikisha inapanga gharama za usafiri wa anga kwa kuzingatia hali halisi ya maisha ya wananchi, badala ya kupanga bei zisizoendana na uwezo wa Watanzania.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Devid Kihenzile, wakati akizungumza na viongozi wa TCAA jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ni muhimu mamlaka hiyo kuweka mfumo wa upangaji wa nauli unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wengi zaidi.
Pia ameielekeza TCAA kuandaa mkakati wa kuongeza idadi ya ndege nchini kupitia uwekezaji wa sekta binafsi, akibainisha kuwa Tanzania ina mazingira salama ya anga pamoja na viwanja vya ndege vya kutosha vinavyoweza kuhudumia ongezeko la safari.
“Hatuwezi kukubali viwanja tulivyovijenga kwa gharama kubwa vitumike mara moja tu kwa siku. Ndege ikitua asubuhi, wafanyakazi wanaenda kulala. Hayo ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma,” amesema Kihenzile.
Amesema idadi ya ndege zilizopo kwa sasa haitoshelezi mahitaji ya soko, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga, ambapo takwimu zinaonesha kuwa idadi ya abiria imeongezeka kutoka 4,200,000 mwaka 2020 hadi 8,100,000 mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Kihenzile, amesema ongezeko hilo linaashiria kuimarika kwa sekta ya usafiri wa anga nchini na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji, watalii na wafanyabiashara katika kutumia anga la Tanzania.
“Ongezeko hili linaonyesha dunia inapenda kuja Tanzania na kutumia anga letu. Pia linathibitisha kuwa Watanzania wanazidi kuchagua usafiri wa anga kama njia ya haraka ya kusafiri ndani na nje ya nchi,” amesema.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameagiza TCAA kuweka mazingira bora yatakayowezesha wawekezaji katika sekta ya anga kupata tija, huku ikihakikisha gharama za huduma zinakuwa nafuu na ubora wa huduma unaendelea kuimarishwa.