
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kujitolea kikamilifu katika kulinda maslahi yake ya kitaifa na usalama wake, akisisitiza kuwa ukosefu wa utulivu wa sasa katika Lango Bahari la Hormuz ni matokeo ya moja kwa moja ya ukiukaji wa ahadi na jinai zilizofanywa na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akizungumza katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, kando ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) nchini Kyrgyzstan siku ya Ijumaa, Araghchi ametoa shukrani zake kwa hatua ya Russia kulaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran.
Aragchi amekumbusha nia njema ya Iran wakati wa mazungumzo yaliyopelekea kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha vita. Aidha amesisitiza kuwa “kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyoonyesha nia ya dhati katika diplomasia, vivyo hivyo imedhamiria kulinda maslahi yake ya kitaifa na usalama wake, na kuzuia Marekani kutumia vibaya Lango Bahari la Hormuz kutishia usalama wa taifa la Iran.”
Kwa upande wake, Lavrov amebainisha tena msimamo wa kimsingi wa Russia unaolaani uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na kujenga uaminifu ili kuweka utaratibu wa usalama wa kikanda unaoongozwa na nchi za eneo la Asia Magharibi.
Mawaziri hao wawili walipitia wamekubaliana kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa hapo awali kati ya Tehran na Moscow.
Aidha wamebadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya eneo la Asia Magharibi kufuatia hatua ya Washington kukiuka tena makubaliano ya kusitisha vita ya Islamabad.
Vita haramu vya uvamizi vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, vilivyoanza tarehe 28 Februari, vimeingia mwezi wa tano.
Mnamo tarehe 8 Aprili, baada ya siku 40, kutokana na operesheni za kulipiza kisasi za Iran na udhibiti wake juu ya Lango Bahari la Hormuz, Marekani na utawala wa Kizayuni walilazimika kukubali makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hata hivyo, Marekani ilianzisha tena mashambulizi yake dhidi ya Iran baada ya kukiuka Makubaliano ya maelewano ya tarehe 17 Juni yaliyosimamiwa na Pakistan.
Jeshi la Marekani limeendesha mashambulizi ya anga kote Iran kwa usiku 13 mfululizo, likilenga maeneo ya raia ikiwa ni pamoja na miundombinu ya mawasiliano, madaraja na mitambo ya kusafisha maji ya chumvi, na kuua watu 55 na kujeruhi wengine 645.
Kujibu mapigo hayo, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vimevurumisha droni na makombora dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo.