Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimefyatua makombora na kupiga kituo kikuu cha kijeshi cha anga katika jimbo la Asir, kusini mwa Saudi Arabia, ikiwa ni hatua ya kujibu mapigo dhidi ya mashambulizi ya kijeshi ya hivi karibuni ya utawala wa Saudia pamoja na mzingiro unaoendelea dhidi ya nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa makombora ya balistiki yaliyotengenezwa nchini Yemen yamelenga na kupiga kwa usahihi maeneo yaliyokusudiwa ndani ya Kituo cha Jeshi la Anga cha Mfalme Khalid (King Khalid Air Base) karibu na mji wa Khamis Mushait, uliopo takriban kilomita 884 kusini mwa mji mkuu Riyadh, mapema Jumamosi.

Inaripotiwa kuwa shambulio hilo limetekelezwa kama jibu kwa uvamizi endelevu wa kijeshi wa utawala wa Riyadh na mzingiro wa kinyama dhidi ya watu wa Yemen.

Hatua hii imekuja muda mfupi baada ya Vikosi vya Ulinzi vya Yemen kushambulia kituo cha mafuta cha shirika la taifa la petroli na gesi asilia la Saudi Arabia, Saudi Aramco, katika jimbo la mpakani la Jizan lililopo kusini-magharibi mwa nchi hiyo, kwa kutumia makombora kadhaa ya balistiki.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa baadhi ya maeneo ya Jizan yalikumbwa na hitilafu na kukatika kwa umeme kufuatia mashambulizi hayo ya makombora.

Aidha, milipuko mikubwa ilitingisha mji wa bandari wa Yanbu nchini Saudi Arabia, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Yemen.

Mifumo ya ufuatiliaji wa safari za ndege kwa wakati halisi (live flight trackers) ilionyesha kuwa ndege zilizokuwa zikielekea Riyadh na miji mingine zililazimika kubadili uelekeo baada ya majeshi ya Yemen kuanzisha mashambulizi hayo dhidi ya Saudi Arabia.

Kutokana na hali hiyo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanamfalme Abdulmohsen Bin Abdulaziz uliopo Yanbu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Abdullah bin Abdulaziz (unaojulikana pia kama Uwanja wa Ndege wa Jizan) ililazimika kusitisha shughuli zake.

Hapo jana Ijumaa usiku, ndege za kivita za Saudia zilitekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu ya mawasiliano na bohari za mafuta katika mkoa wa kimkakati wa pwani wa Hudaydah nchini Yemen.

Siku ya Jumatatu, Yemen ilitangaza rasmi kuanza kwa “mzingiro wa baharini” dhidi ya Saudi Arabia.

Msemaji wa kijeshi wa Yemen, Jenerali wa Brigedia Yahya Saree, alitangaza kupitia taarifa ya runinga kuwa marufuku ya safari za meli zenye uhusiano na Saudia “imeanza kutumika rasmi kuanzia wakati taarifa hii ilipotolewa.” Jenerali Saree alionya kuwa chokocho yoyote au mashambulizi mapya kutoka kwa Saudia yatakabiliwa na “jibu kali na la pande zote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *