
BONDIA Dorotea Muhoza, ameibuka mshindi dhidi ya Debora Mwenda baada ya kushinda kwa uamuzi wa majaji wawili katika pambano la Dar Boxing Derby lililofanyika kwenye Ukumbi wa EACLC, Ubungo, Dar es Salaam.
Dorotea aliondoka na ushindi huo baada ya majaji kutoa pointi za 75-76, 77-75 na 74-79 matokeo yaliyoonyesha namna pambano hilo lilivyokuwa na ushindani mkubwa.
Debora alianza pambano kwa kasi akitumia ngumi za mbele kumuweka chini ya presha mpinzani wake, lakini Dorotea alionyesha utulivu mkubwa, akitumia mashambulizi ya kushtukiza na kujilinda vizuri, hali iliyowashawishi majaji wawili kumpa ushindi baada ya raundi zote kukamilika.
Ushindi huo ni muhimu kwa Dorotea ambaye kabla ya pambano hilo alikuwa na rekodi ya mapambano saba, akishinda moja na kupoteza sita, huku ushindi mmoja aliupata dhidi ya Egine Kayange mwaka 2021.
Kwa Debora kabla ya pambano hilo alikuwa amepigana mara sita, akishinda mapambano matatu, akipoteza mawili na sare moja, rekodi inayomfanya kuwa mmoja wa mabondia wa kike wanaotarajiwa kufanya makubwa nchini.
Licha ya kupoteza, Debora alipambana kwa moyo mkubwa na kuwafanya mashabiki washuhudie pambano la kuvutia, huku kila bondia akipata nafasi ya kutawala baadhi ya raundi kabla ya uamuzi wa mwisho kutolewa.
Pambano lingine la wanawake lililoshuhudiwa viwanja hivyo, Sarah Alex ameendeleza ubabe wake baada ya kumshinda Dorisia Mazige kwa uamuzi wa majaji (unanimous decision).
Sarah alitawala karibu raundi zote za pambano hilo na kuwashawishi majaji wote watatu waliompa ushindi kwa pointi 78-73, 77-74 na 78-73, matokeo yaliyoonyesha ubora wake wa kushambulia na kumiliki pambano kuanzia mwanzo hadi mwisho.