YANGA haitanii na sasa mabosi wa juu wako mezani na mshambuliaji hatari Peter Shalulile wakitaka aongezwe kwenye usajili wa msimu ujao ingawa wanakutana na upinzani kutoka kwenye klabu nyingine kubwa barani Afrika.
Yanga inataka Shalulile ambaye amewahi kufanya kazi na kocha Manqoba Mngqithi kumuongeza kwenye kikosi chao cha msimu ujao kazi ambayo juzi ilikuwa ikifanywa na Rais wao Hersi Said aliyekuwa nchini Afrika Kusini.
“Tumefanya mazungumzo na Yanga kweli, tulikuwa tunaongea na Rais wa klabu hiyo, ni mtu mzuri sana na mazungumzo yetu yanakwenda vizuri,” amesema mmoja wa wasimamizi wa mshambuliaji huyo.
“Tunakwenda vizuri, ukiniuliza tumefikia wapi ni kama asilimia 70 hivi bado mambo machache sana, hakuna shida unajua hata mchezaji amefurahishwa kwani atajiunga na kocha ambaye amewahi kufanya naye kazi.”
Shalulile raia wa Namibia, amemaliza mkataba wake na Mamelodi na sasa anatafuta changamoto mpya sehemu nyingine akiwa na ofa nyingi mezani kutoka mataifa ya Zimbabwe na hapo hapo Afrika Kusini.
Shalulile (32) ni mshambuliaji aliyeweka rekodi kubwa nchini Afrika Kusini, akiwa na MamelodinSundowns ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika.
Mshambuliaji huyo amedumu kwa miaka sita ndani ya Mamelodi akicheza mechi 178 akifunga jumla ya mabao 92 na asisti 22.
Shalulile ana rekodi kubwa akiwa ameshachukua tuzo ya ufungaji bora kwa misimu mitatu akiwa ni mchezaji pekee aliyewahi kufanya hivyo tangu atue Mamelodi akitokea Highlands Park ya hapo hapo Afrika Kusini.
Yanga inataka kumpa mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji huyo wenye kipengele cha kuongeza mwingine, wakitaka kupima ufanisi wake.