YANGA imetambulisha wachezaji wake watatu wapya wa kigeni akiwemo mshambuliaji na viungo wawili washambuliaji, ikiendelea kuboresha kikosi chake kuelekea msimu wa 2026-2027.
Akitangaza kwenye mkutano maalum usiku wa Julai 24, 2026, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said amesema baada ya usajili wa wachezaji wa ndani, klabu hiyo inatafuta wachezaji watano wa kigeni kwenye maboresho ya kikosi.
Hersi amesema katika wachezaji hao watano wa kigeni, wamemsajili mshambuliaji Cheikh Ibrahima Toure raia wa Ufaransa mwenye asili ya Senegal.
Tours anatua Yanga akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na Al Jabalain FC ya Saudia alikocheza kwa mara ya mwisho.
Mshambuliaji huyo aliyesaini miaka miwili ndani ya Yanga, amewahi pia kucheza Ligi ya pili nchini Ufaransa akiitumikia AS Nancy.
Hersi pia amemtangaza viungo wawili washambuliaji akiwemo Housseine Zakouani ambaye ni raia wa Comoro aliyezaliwa Ufaransa.
Zakouani ameitumikia Al Zulfi ya Saudi Arabia akitua Yanga kama mchezaji huru, ambapo anamudu kucheza winga ya kulia.
Yanga pia imemtambulisha winga wa kushoto, Mzambia Albert Kangwanda, aliyeitumikia Red Arrows ya kwao.
Wachezaji hao wametambulishwa rasmi kwenye mkutano huo tayari kwa kuanza kazi kujiandaa na msimu ujao wakati huu ambapo mazoezi ya timu hiyo yanaendelea kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Hersi ameongeza kuwa, bado hawajamaliza usajili wakisalia kutambulisha wachezaji wawili wa kigeni wenye ubora mkubwa ambao muda wowote watawekwa wazi.
Utambulisho wa wachezaji hao, unafanya Yanga hadi sasa kuwaweka hadharani nyota wapya tisa wakiwemo wazawa sita ambao ni Juma Issa Abushiri kutoka Fountain Gate, Hussein Mihambo (Mashujaa), Abdulnasir Muhamed (Mashujaa), Mohamed Mussa (Mashujaa), Erick Mwijage (Mashujaa) na Suleiman Mbarouk maarufu Mpemba D aliyekuwa JKU.