
Canada. Kisa kilichoripotiwa hivi karibuni kinachukiza, kufikirisha, kufundisha na hata kufichua uamuzi wa ovyo, mila na utamaduni wa ovyo.
Wengi, ama kwa kusahau au kutojua, walishangazwa na kisa cha baba mkwe kumuoa mkamwana wake. Mbona yapo mengi japo yanafichwa.
Katika nchi yetu na Afrika kwa ujumla, kuna mila kama hizi tena zinazofumbiwa macho au kutoitwa jina lake kamili yaani uchafu, uchoyo, na ufuska.
Haiingii akilini kwa mtu asiye mchafu na mchoyo kufikiri, kutamani, achia mbali kuoa mkamwana au kuolewa na mkwe kama iivyoripotia.
Leo, tutadurusu kadhia hii ambayo inaanza kuwa gonjwa la kijamii. Wakati tukishangaa baba mkwe kumuoa mke wa mwanae, yaani mkamwana, tujiulize. Je, haya hayapo?
Si chuki wala uzushi, kuna makabila yanayofanya na kuvumilia mambo haya. Mfano, hatushangai kuona mtoto akifanana na babu yake kuliko baba yake? Katika makabila yenye utamaduni wa watoto kuoa na kuwaacha wake zao vijijini na wazazi wao, mbona hili ni jambo la kawaida! Mbona siyo siri kukuta baba mkwe akimtunza mkamwana kuliko hata mkewe?
Kwa watu maarufu, kisa cha baba mkwe kutembea na mkamwana wake hadi kuvunja ndoa ya mwanae kilitokea nchini Nigeria ambapo rais wa zamani wa nchi hiyo Olusegun Obasanjo alishitakiwa na mwanae akimtuhumu kutembea na mkewe.
Kwa mjibu wa BBC (Aprili 3, 2008), mtoto wa Obasanjo aitwaye Gbenga kupitia kiapo, alifungua kesi akimshitaki baba yake kwa kutembea na mkewe aitwaye Mojisola alikubali kutembea na baba mkwe wake ili kupata tenda serikalini.
Mbali na kashfa ya Obasanjo, binafsi, tuliwahi kushuhudia kashfa ambapo mama alikuwa akitukanana na binti yake baada ya binti kuachwa na mpenzi wake na kuchukuliwa na mama yake. Ni uchafu na uhayawani kiasi gani kuendekeza tamaa kiasi hiki?
Ukiachia mbali kashfa hizo hapo juu, zipo kashfa nyingine ambazo huvishwa joho la mila. Kuna makabila nchini mwetu ambayo huruhusu kurithi wajane.
Utakuta mwana akiwarithi wake wa baba yake anapokufa au shemeji kuridhi mke wa kaka yake. Je, kama hawa wanaweza kurithishana hivi, ni kitu gani kitawazuia kuchukuana?
Kwa wenyeji wa baadhi ya mikoa mambo kama hayo hapo juu ni ya kawaida. Hawakatai watoto ambao wake zao wamezaa na watu wengine wakiwa katika ndoa.
Kwao, ni kwamba kitanda hakizai haramu japo kinazaa haramu au mtoto au watoto husika huzaliwa kwenye ‘ng’ombe’ wao, yaani mahari ya ng’ombe walizotoa.
Ajabu ya maajabu, uchafu na ufuska huu huitwa mila. Mila gani zaidi ya uchafu na ufuska?
Katika hali ya kawaida kwa mtu mwenye akili timamu na kujali haki na utu wa wengine, unawezaje kumtamani mkwe au mkamwana wako?
Sambamba, kuna kabila moja la kaskazini linalojulikana kwa tabia hizi. Utakuta mkamwana kazini na kuzaa na baba mkwe wake na mtoto aliyezaliwa mle akiitwa anko na wale wanaopaswa kumuita mtoto wa baba mkubwa au baba mdogo. Ajabu na tabia ya ufuska, balaa kama hili linafunikwafunikwa.
Yupo mmoja aitwaye Jerome (si jina lake halisi) sasa mtu mzima mwenye mke na watoto tunayemjua. Jamaa huyu alizaliwa wakati baba yake akiwa masomoni Ulaya.
Baada ya baba mkwe kumzaa na mkamwana wake, mume wake aliporejea na kumkuta mtoto ambaye hakuwa amemzalisha, aliamua kumuacha mke hapo hapo. Baba mtu alimchukia na kuamua kuwatunza mama na mtoto kwa vile anajua alichokuwa amefanya.
Wakati tukishangaa hayo hapo juu, pia, yapo makabila ambapo ndugu kwa ndugu huchukuana. Kwa wasiojua hasa wasiotoka kwenye makabila yenye mila chafu kama hizi, kila mwanaume wa kabila la mke ajaye kumtembelea huitwa anko na watoto wa mzinzi husika.
Ukiona hivi, jua vyako vyaliwa. Ndiyo maana, katika safu hii, tumekuwa tukisisitiza waoaji wawe makini na watu wanaowaoa au kuolewa nao. Hii ni kutokana na ukweli kuwa makabila yenye mila hizi chafu yanajulikana.
Tumalize kwa kukemea uchafu huu ambao ni mbaya kuliko uchafu wowote, kwa vile unaumiza wengi tena wasio na hatia. Unapovunja ndoa ya wenzio, unawaumiza maisha yao yote.