Kibaha. Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala zake kwa kuwapatia mafunzo ya uongozi yanayolenga kufungamanisha utendaji wa taasisi hizo na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Miongoni mwa walioshiriki mafunzo hayo ya siku nne ni Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji (TPRB), Martha Mkupasi.
Mafunzo hayo yameanza leo Jumamosi Julai 25, 2026 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, ambapo yameaandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Kutoka Maono Mpaka Matokeo: Kufungamanisha Utekelezaji wa Mashirika ya Umma na Dira 2050.”
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mkupasi amesema yamewapa viongozi mbinu za kuoanisha maono ya Taifa na utekelezaji wa majukumu ya kila siku ili mipango ya taasisi iwe na mchango wa moja kwa moja katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ame sema washiriki pia wamejifunza namna ya kuendesha taasisi kwa kuzingatia matokeo, kuimarisha uwajibikaji, kupanga kwa ufanisi na kukuza ubunifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Maarifa tuliyoyapata yataongeza ufanisi wa taasisi za umma na kusaidia kuhakikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi,” amesema.
Mafunzo hayo yanakuja wakati Serikali ikiwa imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo ilizinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 17, 2025, ikiwa ni mwongozo mkuu wa maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
Dira hiyo inalenga kujenga Tanzania kuwa taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea, huku ikisisitiza uchumi shindani, matumizi ya teknolojia na ubunifu, maendeleo ya rasilimali watu pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali za taifa.
Wakati wa uzinduzi wa Dira hiyo, Rais Samia aliagiza taasisi zote za umma kuhakikisha zinaoanisha mipango, bajeti na utekelezaji wake na malengo ya Dira 2050. “Mafanikio ya Dira hayatapimwa kwa ahadi au maelezo, bali kwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi, uwajibikaji, ufuatiliaji wa karibu na upimaji wa utendaji viwe sehemu ya utamaduni wa taasisi za Serikali,” alisema Rais Samia.