
Rais wa Senegal azindua chama chake cha kisiasa baada ya kutengana na mshirika wake wa zamani, Sonko
Hatua hii inatajwa kuzidisha mgawanyiko kati ya Rais wa Senegal na mshirika wake wa zamani aliyegeuka kuwa mpinzani, Ousmane Sonko, ambaye anaongoza chama tawala cha Pastef nchini humo.
Viongozi hao wawili, ambao waliingia madarakani pamoja mwaka 2024 kwa tiketi ya chama tawala, wanatarajiwa kuchuana vikali katika uchaguzi wa rais mwaka 2029.
Wiki kadhaa zilizopita kulizinduliwa vuguvugu la Rais Faye kwa jina la ‘Kiray’ au ‘Republican Patriots’, ambapo maafisa wengi wa chama cha Pastef walijiuzulu katika chama hicho ili kujiunga na kambi ya Rais wa Senegal.
Wakati huo huo wanachama kadhaa wa chama cha upinzani cha Alliance for The Republic pia wamejiunga na chama cha rais, wakiwemo viongozi kadhaa wa ngazi ya mkoa na wanachama wa tawi lake la vijana.
Muungano wa Faye na Sonko ulivunjika kufuatia mivutano kuhusu maamuzi muhimu ya sera.
Mivutano hiyo ni pamoja na namna ya kujihusisha katika mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu mpango wa mkopo kwa nchi hiyo, huku Senegal ikikabiliwa na mgogoro mkubwa wa madeni.
Inafaa kuashiria hapa kuwa Bassirou Diomaye Faye alimuondoa Ousmane Sonko katika wadhifa wa Waziri Mkuu mapema mwaka huu, lakini chama cha Sonko kilidumisha wingi wake mkubwa wa viti vya Bunge na akachaguliwa kuwa Spika wa Bunge muda mfupi baadaye.
Waziri Mkuu mpya wa Senegal, Ahmadou al Aminou Lo, aliteuliwa Mei mwaka huu; hata hivyo baraza la mawaziri iliundwa bila ya kuteuliwa waziri yeyote kutoka chama cha Pastef baada ya Sonko kutangaza kuwa chama chake hakitashiriki serikalini.
Mwaka wa 2024, Faye na Sonko walifanya kampeni kwa pamoja wakiahidi kuandaa ajira kwa vijana, kupambana vikali na ufisadi na kuipatia Senegal sehemu kubwa zaidi ya mapato yatokanayo na utajiri wake wa mafuta, gesi na madini. Lakini ahadi hizo hazijatekelezwa.
Mzigo wa deni la Senegal umeongezeka tangu walipoingia madarakani, baada ya maafisa wa mamalaka husika kugundua kuwa utawala uliopita ulikuwa umeficha mabilioni ya dola katika mikopo iliyochukuliwa.