Mbeya. Zaidi ya Sh45 milioni zimekusanywa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya biashara ya Kanisa Katoliki, Parokia ya Chunya, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Fedha hizo zimepatikana katika harambee iliyo fanyika leo, Julai 26, 2026, baada ya ibada takatifu iliyoongozwa na Padri Sylvester Mpigauzi, huku Mbunge wa  Lupa, Masache Kasaka, akiongoza shughuli ya uchangishaji.

Akizungumza baada ya harambee hiyo, Kasaka amesema ushiriki wa waumini  kuchangia miradi ya maendeleo ya Kanisa ni sehemu ya kuimarisha huduma za kiroho na kijamii.

“Waumini muwe mstari wa mbele kushirikiana na viongozi wa Kanisa katika kuchangia miradi mbalimbali inayoanzishwa. Hilo litakuwa chachu ya maendeleo na sehemu ya ibada yetu,” amesema.

Kasaka pia amewataka waumini kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa hekima, uadilifu na kulinda amani iliyopo nchini.

Amesema harambee hiyo imefanikiwa kukusanya Sh45 milioni, ambapo Sh35 milioni zimetolewa taslimu na Sh10 milioni ni ahadi za michango. Lengo ni kukusanya zaidi ya Sh50 milioni kwa ajili ya kukamilisha mradi wa nyumba hiyo ya biashara.

Kwa upande wa Mpigauzi, amemshukuru Kasaka kwa kukubali kuongoza harambee hiyo na kuhamasisha waumini na wadau mbalimbali waliofanikisha kupatikana kwa Sh45 milioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *