
Askari usalama wa Iran wamefanikiwa kuwatambua na kuwakamata vinara 140 waliohusika katika machafuko ya karibuni hapa nchini kwa ufadhili na kuungaji mkono na nchi za nje. Vinara hao wa ghasia za karibuni wametiwa nguvuni katika mji wa Hamedan, magharibi mwa Iran.
Idara ya Intelijinsia ya mji wa Hamedan imearifu kuwa wote waliotiwa nguvuni wana uhusiano na utawala wa Israel, mtandao wa kigaidi wa kimataifa na mitandao inayohusika na utengenezaji na usambazaji wa mabomu na silaha za kurusha kwa mkono.
Mmoja wa magaidi hao, ambaye alifika Hamedan kutoka mkoa jirani kwa nia ya makusudi ya kusababisha uharibifu, alikimbia na kujificha katika kaunti ya Mkoa wa Tehran baada ya kumuua afisa wa usalama.
Mhalifu huyo alikamatwa katika oparesheni ya pamoja ya intelijinsia na utendaji kazi ya polisi kwa ushirikiano na wananchi.
Mhalifu huyo aliyemuua afisa wa usalama ana rekodi ya kutenda jinai ikiwa ni pamoja na kutiwa hatiani kwa utekaji nyara na shambulio la kukusudia.
Wakati huo huo watu kadhaa waliohusika katika shambulio la kikatili dhidi ya vikosi vya kujitolea vya wananchi, Basij, huko Hamedan na kumshambulia mpita njia mzee huko Nahavand, wametambuliwa na kukamatwa.
Idara ya Intelijinsia ya mji wa Hamedan imesema kuwa imezitambua pia timu mbili zilizokuwa zikizalisha na kusambaza mabomu ya kurusha kwa mkono katika maeneo ya ghasia. Katika msako huo, polisi imenasa idadi kubwa ya mabomu hayo na zana zinazotumika kuzalishia mabomu hayo.
Idara ya Intelijinsia ya mji wa Hamedan pia imekamata timu tatu za watu wanne ambao walihusika katika uharibifu wa mali na magari ya umma na ya watu binafsi, raia wawili wa kigeni, ajenti mwenye uhusiano na Israel na timu iliyounganishwa na mtandao wa kimataifa wa kigaidi.