Maafisa na wachambuzi wa Israel, wameonya kuhusu matokeo mabaya ya mzozo wowote na Iran, wakisisitiza kwamba nguvu ya makombora na uwezo wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ni changamoto kubwa kwa Tel Aviv na kwamba Israel haipaswi kupuuzwa ukweli huo.
Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Olmert, amekosoa kauli za Waziri Mkuu wa sasa kuhusu Iran, akisema kwamba kutia chumvi kwa Netanyahu hakuongezi chochote kwenye usalama wa Israel. Ehud Olmert amesisitiza kwamba kauli hizo zinaunda matarajio bandia tu na kutia watu wasiwasi.
Olmert amesema kwamba Israel haitaanzisha shambulio la awali dhidi ya Iran, akiongeza kwamba uwezo wa Israel haupaswi kutiwa chumvi na kwamba haipaswi kudhaniwa kwamba utawala huu unaweza kuiteteresha Iran.
Amesema kwamba hata Marekani ilikuwa na wasiwasi kuhusu suala hilo, kwa sababu kushambulia Iran kungezidisha hali mbaya ndani ya Marekani. Ehud Olmert ameongeza kuwa, gharama ya kushambulia Iran ni “nzito sana” na hakuna haja ya jamii ya Israel kuingia “katika hali ya hofu isiyo ya lazima.” Olmert pia ameutaja muungano tawala kuwa “kundi la wanasesere.”
Wakati huo huo, Avigdor Lieberman, Waziri wa zamani wa Vita wa Israel, amesema kwamba Iran imeonyesha tena kina cha tishio lake kwa kulenga shabaha za kimkakati za Israel, ikiwa ni pamoja na shambulio kwenye kambi ya Nevatim.

Lieberman ameongeza kuwa: “Ni vigumu kutabiri shabaha zijazo za mashambulizi ya Iran na kuzihamisha mapema.” Amesema, baada ya Vita vya Siku 12, Iran imeongeza ubora wa makombora yake ya balestiki na imeweza kutengeneza mamia ya makombora mapya.
Lieberman amesema kwamba kile kilichofanywa na makombora ya Wairani kwenye Taasisi ya Weizmann, ni kikubwa zaidi ya uharibifu wote mbaya, na kwamba shambulizi hilo liliharibu kila aina ya data na matokeo muhimu sana na miongo kadhaa ya utafiti.