
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema kuwa utawala wa Israel umeshindwa kwa fedheha kubwa zaidi katika ghasia za kigaidi zilizotokea hivi karibuni nchini Iran ikilinganishwa na vita vya siku 12 vya kulazimishwa vya mwezi Juni mwaka jana.
Qalibaf alisema Jumamosi kwamba, “Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulizi ya kigaidi yaliyopangwa na kufanywa kwa wakati mmoja katika miji mbalimbali ya Iran, lakini… ndani ya muda usiozidi saa 48 umepata fedheha kubwa zaidi kuliko ile ya vita vya siku 12.”
Mwezi Juni waka jana, utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa himaya ya Marekani, ulianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran na hatimaye baada ya siku 12, utawala huo ulilazimika kuomba usitishwaji vita.
Qalibaf amesifu juhudi kubwa za Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika kulilinda taifa, iwe wakati wa vita vya Marekani na Israel au katika ghasia za kigaidi zilizotokea hivi karibuni.
Ameongeza kuwa ghasia hizo zilizopewa nguvu na tawala hasimu za ya kigeni zilifanana na mbinu za kundi la kigaidi la Daesh (ISIS), lililojulikana kwa uhalifu na mauaji, na kwamba wahusika wa ghasia hizo hawakuwa na imani wala heshima kwa dini.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa magaidi hao walipatiwa mafunzo kikamilifu na utawala wa Israel, Marekani, na washirika wao.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Qalibaf ametoa onyo kuhusu njama za maadui za kuibua mgawanyiko ndani ya nchi ili kudhoofisha maslahi ya taifa la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesisitiza umuhimu wa kufuata maelekezo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatulah Seyyed Ali Khamenei, kama njia ya kukabiliana na njama za mahasimu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, matatizo ya kiuchumi yaliyosababishwa na kuongezwa kwa miaka mingi ya vikwazo vya Magharibi yalichochea wimbi la maandamano ya amani miongoni mwa wafanyabiashara wa Tehran na miji mingine.
Mamlaka zilikiri kuwa madai ya waandamanaji yalikuwa halali, lakini maandamano hayo yalitekwa na wahuni walioungwa mkono na viongozi wa Marekani na Israel, ambao walitoa wito wa wazi wa uharibifu na vurugu.
Maafisa walisema kuwa baadhi ya mamluki walikuwa wamejihami, wamefunzwa, na kuajiriwa na mashirika ya kijasusi ya Marekani na Israel kwa lengo la kuchochea ghasia, kuharibu mali ya umma, na kuua raia pamoja na wanajeshi wa usalama.