Wananchi wa Sweden wamefanya maandamano mengine katika mji mkuu wa nchi hiyo, Stockholm, kulaani mashambulizi ya Israel yanayowalenga Wapalestina katika Ukanda wa Gaza licha ya kufikiwa mapatano ya usitishaji vita.

Waandamanaji walitembea katika mitaa mbalimbali ya Stockhom wakitaka kusitishwa jinai zote za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebebe bendera za Palestina na mabango yenye maandishi ya kulaani jinai na mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza. 

Katika maandamano hayo, Rana Kadri, mwanaharakati Msweden mwenye asili ya Palestina amesema kuwa mashambulizi ya Israel yanazidisha maafa ya binadamu huko Gaza.

Kadri ameongeza kuwa watoto wachanga wa Kipalestina wanaaga dunia huko Gaza kutokana na baridi si kwa sababu hali ya hewa ni baridi sana bali kutokana na kwamba wanajeshi wa Israel wanaendelea kuzuia kuingizwa bidhaa muhimu za mahitaji na misaada ya kibinadamu kama dawa, mavazi na mablanketi katika Ukanda wa Gaza.  

Wapalestina zaidi ya 71,000 wameuliwa shahidi  na maelfu ya wengine wamejeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza Oktoba 2023. 

Aidha  Wapalestina zaidi ya 171,000 wamejeruhiwa katika vita hivyo vya Israel vilivyoifanya Gaza kuwa mji wa magofu. Wahanga wengi wa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza ni watoto wadogo na wanawake. 

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa jeshi la utawala ghasibu wa Israel linaendelea kuwashambulia Wapalestina licha ya usitishaji vita ulioanza kutekelezwa tarehe 10 Oktoba mwaka jana, na hadi sasa limeuwa takriban Wapalestina 500 na kuwajeruhi wengine 1,313 huko Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *