Leo tunafuatilia nyayo za kuhusika Marekani na Israel katika ghasia na machafuko ya karibuni nchini Iran..
Baada ya kutulia ghasia na machafuko katika miji mingi ya Iran mwanzoni mwa mwaka mpya, sasa ni fursa ya kuchunguza mizizi na chanzo cha ghasia hizo zilizoandamana na ukatili mkubwa. Kitu ambacho kimezidi kuwa dhahiri kadri muda unavyopita na kutokana na mkusanyiko wa data, taarifa na ripoti za vyombo vya habari ni nafsi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kupanga, kuzidisha na kuchochea machafuko hayo. Uingiliaji kati huo wa Marekani na Israel sio simulizi kutoka kwa maafisa na vyombo vya habari vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pekee kuhusu mizizi na chanzo cha machafuko ya hivi karibuni nchini Iran. Bali mkusanyiko mzito wa maungamo ya wazi, misimamo ya umma, ripoti za vyombo vya habari vya Magharibi, na ushuhuda wa uwanjani umethibitisha kwamba uingiliaji kati huo ni ukweli usiopingika. Uchunguzi wa nyayraka hizo unaonyesha kwamba machafuko ya hivi karibuni nchini Iran yalikuwa sehemu ya mradi wenye tabaka kadhaa na uliopangwa. Mradi huo ulipanda mawimbi ya malalamiko halali ya baadhi ya wananchi wa Iran kuhusu hali ya kiuchumi ambapo uingiliaji kati wa baadhi ya madola ya kigeni umebadilisha malalamiko hayo kuwa vurugu zisizo na msingi, uharibifu mkubwa wa mali ya umma, na kuua raia na askari usalama.

Rekodi ya kihistoria ya uingiliaji kati wa Marekani na washirika wake nchini Iran inatoa fremu ya kwanza ya uchambuzi wa kuelewa matukio hayo. Uingiliaji kati wa Marekani nchini Iran ulianza kwa mapinduzi ya Agosti 19, 1953, kwa ushirikiano wa moja kwa moja wa shirika la ujasusi la nchi hiyo, CIA na shirika la ujasusi la Uingereza, kwa lengo la kuipindua serikali ya kitaifa ya Dkt. Mohammad Mossadegh. Uingiliaji kati huo uliendelea kwa miongo kadhaa ya kuunga mkono utawala wa kidikteta na wa kiimla wa Pahlavi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Marekani ilijaribu kuweka vikwazo vikali, kumtumia Saddam Hussein kushambulia Iran katika miaka ya 1980, na kulazimisha vita vya miaka minane. Kuendelezwa uhasama na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumekuwa sehemu thabiti ya mkakati wa sera za kigeni za Marekani. Utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao unatambua kwamba usalama na kubakia kwake hai kumo katika kuidhoofisha Iran, mara nyingi umeelekeza sera ya kigeni ya Marekani upande wa kuwa na uadui dhidi ya Iran kwa msaada wa kundi la Lobi za Wazayuni nchini Marekani.

Kwa hivyo, machafuko ya hivi karibuni nchini Iran yanapaswa kuonekana kama mwendelezo wa muundo huu wa kihistoria. Ni mfano unaokaririwa nyakakati zote kwa kutumia zana na simulizi mpya, lakini lengo lake kuu, yaani kuteteresha na kudhoofisha Iran, linabaki kuwa thabiti. Taarifa za waziwazi na ambazo hazijawahi kutokea za baadhi ya maafisa na watu mashuhuri wa Magharibi ni mojawapo ya makala muhimu zaidi zilizoandikwa kuhusu uchambuzi huu.
Lawrence Wilkerson, Mkuu wa zamani wa Idara ya Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, anazungumzia waziwazi kuhusu nafasi ya pamojaya Mossad, CIA na MI6 katika matukio ya karibuni nchini Iran na anasisitiza kwamba vitendo hivyo vinafanywa chini ya msaada wa moja kwa moja wa Donald Trump. Maneno haya yanasemwa na mtu ambaye amekuwa kitovu cha mfumo wa sera za kigeni wa Marekani kwa miaka mingi na anajua vizuri mifumo yake ya uendeshaji. Wilkerson anazungumzia waziwazi uwepo wa wageni waliojivika magwanda ya raia wa Iran katika mukusanyiko ya wananchi na nafasi yao katika vurugu na hata mauaji. Suala hili linaweka wazi kwa njia nzuri ni kwa nini matukio mengi ya vurugu hayaoani na mantiki ya maandamano ya kiraia, na yalifanana zaidi na operesheni zilizokuwa zikiongozwa kwa malengo maalumu.
Matamshi ya waziwazi ya baadhi ya maafisa wa serikali na watu mashuhuri wa Magharibi yanaunda tabaka la kwanza la nyaraka hizo. Mkuu wa zamani wa Idara ya Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Lauren Wilkerson anazungumzia waziwazi vitendo vya pamoja vya Mossad, CIA na MI6 nchini Iran, na anasisitiza kwamba vitendo hivyo vinafanywa kwa msaada wa moja kwa moja wa Donald Trump. Anasema kwamba mamluki hao walishirikki kwenye mikusanyiko kama raia wa Iran na wanachochea ukatili na mauaji. Kauli hii si uchambuzi wa mwangalizi wa nje, bali ni ungamo la mtu ambaye amekuwepo katika ngazi za juu zaidi za sera za kigeni za Marekani kwa miaka mingi na anaelewa vyema mifumo inayotumiwa na nchi hiyo kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine.
Katika muktadha huo, Jeffrey D Sachs, Profesa mashuhuri wa Chuo Kikuu cha Columbia, anayataja maandamano ya Iran kama mfano wa “vita maalumu.” Anasema kuwa hicho ni kigezo kilichotumiwa mara nyingi na CIA na Mossad kwa miongo kadhaa. Msisitizo wa Sachs kuhusu “mkakati unaojulikana wa Marekani na Israel” unaonyesha wazi kwamba kilichotokea Iran ni marudio ya hali iliyojaribiwa katika nchi tofauti.
Kukiri vyombo vya habari na maafisa wa utawala wa Israel kunaunda safu nyingine ya nyaraka hizo. Gazeti la Jerusalem Post limezungumzia waziwazi uwepo wa mawakala wa Mossad katika maandamano ya Iran. Kukiri kama huku hutangazwa waziwazi kwa nadra sana katika vyombo vya habari vya Israel, na jambo hili linazidisha maradufu umuhimu wa waraka huu. Yumkini kukiri waziwazi na kwa kushangaza zaidi ni kule kwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo, ambaye, katika ujumbe kwa watu wa Iran, alitangaza uungaji mkono kwa waandamanaji huku akiashiria uwepo wa “mamluki na vibaraka wa Mossad baina ya wandamanaji hao.” Kauli hii ni kukiri waziwazi kuwepo maajenti wa ujasusi wa utawala wa Israel katika machafuko ya Iran na inatosha kuthibitisha uingiliaji kati wa kigeni katika machafuko hayo.
Taarifa za wanajeshi na wataalamu wa masuala ya ujasusi wa Magharibi pia zinakamilisha picha hii. Tamir Morag, mtangazaji wa televisheni ya Channel 14 ya utawala wa Israel, anazungumzia suala la mamluki wa kigeni kusambaza silaha baina ya waandamanaji na kuitaja hatua hiyo kuwa ni sababu ya vifo vya mamia ya watu. Kwa upande wake, afisa wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, Larry Johnson, hayaoni machafuko ya hivi karibuni nchini Iran kuwa uasi wa kawaida na anayaelezea kama hujuma ya kijasusi iliyopangwa na CIA na Mossad.
Douglas Macgregor, kanali mstaafu wa Jeshi la Marekani, anachunguza hatua kwa hatua jinsi maandamano halisi ya kiuchumi yalivyogeuka kuwa mradi wa kijasusi mbapo ndani yake pesa, vifaa vya mawasiliano kama vile Starlink, uchochezi na hata kuhamasisha umma na kuuelekeza kwenye mapigano ya silaha na polisi vilitumika kama zana za kuchochea ukatili. Maelezo haya, hasa yanapotolewa na watu wenye historia ya kijeshi na kiusalama, yanaonyesha kina na uzito wa uingiliaji kati huo.
Uchambuzi wa kinadharia wa John Mearsheimer, Profesa maarufu wa mahusiano ya kimataifa, unaweka wazi zaidi mfumo mkuu wa matukio hayo. Mearsheimer anaona kinachoendelea Iran kinaoana kabisa na “maagizo ya Marekani na Israel” na kuelezea wazi awamu zake. Anasema vikwazo na uharibifu wa kiuchumi ili kuongeza mashinikizo ya kijamii, kuchochea maandamano, kuanzisha kampeni kubwa ya kutoa taarifa potofu ili kuashiria kwamba machafuko hayo ni ya ghafla, na hatimaye kuandaa maoni ya umma kwa ajili ya kuingilia kati moja kwa moja ni sehemu ya mkakati wa Marekani wa kudhoofisha na hatimaye kupindua utawala wa Iran.
Uchambuzi huu unaoana na yaliyojiri nchini Iran na unaweza kufananishwa tajiriba za Iraq, Syria, Libya na nchi zingine. Afisa wa zamani wa CIA John Kiriakou anaashiria jinsi vyombo vya habari vya Israel vilivyojifakharisha kutokana na uwepo wa maajenti wa Mossad baina ya waandamanaji, akionyesha jinsi uingiliaji kati huu unavyotambuliwa na wapangaji wake kuwa jambo la kawaida na halali.
Mbali na kauli hizi, misimamo ya wanasiasa na wasomi huru duniani kote pia inapaswa kupewa mazingatio. Cenk Uygur, Mkurugenzi wa mtandao wa TYT wa Marekani, anasema wazi kwamba, Marekani na Israel hazitaki demokrasia nchini Iran, bali lengo lao ni kusimika kibaraka wao nchini Iran. Uchambuzi huu unatiwa nguvu na historia ya uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa tawala za kimabavu katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Rais wa Serbia, Aleksandar Vučić, yeye amekumbuka mapinduzi ya 1953 nchini Iran yaliyoongozwa na CIA na Uingereza, na kutahadharisha juu ya uwezekano wa kukaririwa jaribio la kama hilo. Vučić pia anawatole wito wananchi wa Iran wasome kitabu “Operesheni Ajax” kinachohadithia Mapinduzi ya CIA yaliyoweka ramani mpya ya Mashariki ya Kati.
Hamid Dabashi, Carl Niehaus na Alastair Crooke pia, kila mmoja kutokana na mtazamo tofauti lakini kwa hitimisho la pamoja, wanazungumzia uwepo wa mamluki wa kigeni waliopewa mafunzo maalumu miongoni mwa waandamanaji wa Iran katika machafuko ya karibuni.
Ripoti Financial Times ya Uingereza inakamilisha sehemu ya nyanjani ya nyaraka zinazothibitisha uingiliaji kati wa Marekani na Israel katika machafuko ya Iran. Simulizi za mashahidi za kuwepo wanaume waliokuwa wamevaa nguo nyeusi, waliokuwa wamejizatiti kwa zana za kutosha, na wanaofanana na makomandoo, ambao walikuwa wakichoma moto kwa makusudi, wakiharibu mali za umaa na za binafsi na kuchochea ukatili na machafukko, zinaonyesha kwamba vurugu hizo hazikuwa matokeo ya mihemko, bali matokeo ya harakati na hujuma zilizopangwa. Maajenti hao waliichanganyika na waandamanaji halisi, wakifanya kile kinachojulikana katika fasihi ya masuala ya usalama kama “utekaji nyara wa maandamano ya amani.” Kwa maana ya kubadilisha asili ya mkusanyiko wa amani kuwa ghasia za vurugu ili kufikia malengo ya kisiasa ya madola ya kigeni.
Kwa ujumla ni kwamba, kuwekwa pamoja ushahidi, taarifa na ripoti hizi kunaonyesha kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zilikuwa na nafasi kubwa katika machafuko ya hivi karibuni nchini Iran. Msaada wa kisiasa na vyombo vya habari, harakati za ujasusi, mipango ya uwanjani, na kuchochea vurugu vyote vimekuwa sehemu ya mradi mmoja wa uingiliaji kati unaolenga kuivuruga Iran na kuzidisha gharama za masuala ya usalama na kijamii kwa nchi hiyo.