
Waziri wa Afya wa Sudan, Dkt. Haitham Mohamed Ibrahim, ameeleza hali ya kiafya nchini Sudan baada ya miaka mitatu ya vita, akisisitiza kuwa hali imeboreka kiasi katika baadhi ya majimbo ikilinganishwa na changamoto kubwa zinazoendelea kushuhudiwa magharibi mwa Sudan na Kordofan.
Dkt. Haitham Mohamed Ibrahim ameeleza kwamba hali ya afya nchini Sudan imeboreka kiasi katika majimbo ya kaskazini na mashariki, ambapo huduma za afya na maalumu zimeimarika.
Kwa upande mwingine, majimbo ya magharibi mwa Sudan na Kordofan yanakabiliwa na matatizo makubwa katika kupata huduma za msingi kwa watu, hasa akina mama na watoto, na katika hali za dharura na lishe.
Kuhusu idadi ya watu waliouawa katika vita vya ndani hadi sasa, Dkt. Haitham amesisitiza kwamba ni vigumu kubaini idadi kamili ya wahanga wa vita kutokana na wigo mpana wa mgogoro huo, akieleza kuwa idadi ya vifo vilivyosajiliwa na taasisi za afya imezidi visa 33,000 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Amesema, zaidi ya miili 4,000 ilizikwa upya Khartoum kupitia kamati ya pamoja ya tiba ya uchunguzi wa kimatibabu, ulinzi wa raia na mamlaka husika, huku idadi ya miili ikiwa ndogo katika majimbo mengine kama vile Al-Jazirah na Sennar.
Waziri wa Afya wa Sudan amezungumzia pia suala la ukatili wa kingono uliofanywa wakati wa vita, akisisitiza kwamba wizara hiyo imekuwa ikiwasaidia waathiriwa wa ukatili huo kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa, vitengo vya afya na vituo maalumu. Amesema jumla ya visa 1,152 vya ukatili wa kingono vilirekodiwa hadi mwisho wa 2025, hasa Kaskazini mwa Darfur, huku takriban mimba 320 zikihitaji uingiliaji kati wa haraka wa kimatibabu.
Waziri huyo almekanusha ripoti za utumiaji wa silaha za kemikali au kibiolojia huko Khartoum au kwingineko, akieleza kuwa Mamlaka Kuu ya Tiba ya Uchunguzi wa Kisheria, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, na Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma hazijagundua vifo vya halaiki vya watu au uchafuzi wa kemikali. Ameeleza kwamba baadhi ya malalamiko kuhusu gesi ya klorini yalitokana na utumiaji wa dawa za kuua vijidudu na haukuwa na athari yoyote ya sumu kwa raia.