
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa, serikali ya Marekani inakandamiza vyombo vya habari na kuvizuia kueleza ukweli.
Taarifa ya Amnesty International imetoa wito kwa mamlaka za Marekani kuwaachilia huru mara moja waandishi wa habari waliokamatwa wakati walipokuwa wakiripoti maandamano.
Shirika hilo la haki za binadamu limesisitiza kuwa, uandishi wa habari na utangazaji wa maandamano si uhalifu, na kwamba jinsi waandishi wa habari wanavyotendewa ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa kujieleza na haki za vyombo vya habari.
Taarifa hiyo imeashiria kukamatwa Don Lemon, mwandishi wa habari maarufu na mwandishi wa habari wa zamani wa CNN, na Georgia Fort, mwandishi wa habari huru, ambao walitiwa mbaroni walipokuwa wakiripoti maandamano dhidi ya sera za uhamiaji za serikali ya Marekani katika kanisa moja katika jimbo la Minnesota.
Amnesty International imesema: “Kukamatwa waandishi hawa wa habari ni jaribio la kutisha vyombo vya habari na kuzuia kuchapishwa ripoti muhimu kuhusu utendaji wa serikali; vitendo kama hivyo ni ishara ya wasiwasi ya kubinywa nafasi ya vyombo vya habari na shinikizo linaloongezeka kwa waandishi wa habari nchini Marekani.”
Mkurugenzi wa programu wa Amnesty International nchini Marekani pia amekosoa hatua hiyo, akisema kwamba kuwakamata waandishi wa habari kwa kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma ni tishio kubwa kwa haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari, na kunaweza kuwazuia waandishi wengine kuripoti matukio kwa uhuru.
Mwishoni mwa taarifa yake hiyo, Amnesty International imeitaka serikali ya Marekani kukomesha vikwazo na mbinyo dhidi ya waandishi wa habari na kuandaa mazingira ili waandishi wa habari waweze kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma bila hofu ya kukamatwa au kubinywa kiusalama.