WAKATI dirisha dogo la usajili likifungwa rasmi Januari 30, 2026, baada ya kudumu kwa mwezi mmoja tangu lilipofunguliwa Januari 1, 2026, mabosi wa Azam FC wamekamilisha dili la winga nyota, Mnigeria Abel Abah kutokea KF Tirana ya Albania.

Nyota huyo amekamilisha usajili huo mwishoni akiwa ni mchezaji wa tano kusajiliwa na kikosi hicho, akienda kuchukua nafasi ya Mtunisia Baraket Hmidi, aliyeondoka kikosini humo kwa mkopo na kujiunga na Diyala SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq.

Abah anayecheza wingi ya kulia kwa ufasaha akiwa na miaka 23, alijiunga na KF Tirana Julai 4, 2024, baada ya kuondoka FK Metalac Gornji Milanovac ya Serbia, ikiwa ni pendekezo la benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha, Florent Ibenge.

Nyota huyo anaungana na mastaa wengine wapya waliosajiliwa dirisha hili dogo, akiwamo, Ilese Kolonga Caleb aliyetokea Esperance Football Academy, Aimar Hafidh Abubakar ‘Haaland’ (Mlandege FC) na Mzee Hassan Mzee ‘Aziz KI’ kutokea KMKM FC.

Mwingine ni nyota Mkongomani Jean-Jacques Ngita, aliyetokea Aris Limassol FC ya Cyprus, ambaye ameanza vizuri baada ya kuifungia bao moja la Ligi Kuu Bara katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya TRA United, Januari 29, 2026.

Ongezeko la nyota hao ni kuongeza upana na ubora wa kikosi hicho cha kocha, Florent Ibenge kutokana na mashindano ambayo inashiriki msimu huu, ikiwamo ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Kombe la Shirikisho. Barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *