Mamia ya watu wameandamana huko Milan, Italia, kupinga mpango wa Marekani wa kuwatuma maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani, au ICE, kuwalinda washiriki wa Marekani katika Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Milano Cortina.
Januari 31, mamia ya raia walijitokeza mitaani huko Milan, moja ya maeneo ambayo yataandaa Michezo ya Olimpiki ijayo. Baadhi yao walikuwa wamebeba mabango yenye kauli mbiu za kupinga ICE.
Meya wa Milan hapo awali alisema katika kipindi cha redio kwenye eneo hilo kwamba wafanyakazi wa ICE hawatakaribishwa mjini humo.
Maandamano hayo yalitokea huku kukiwa na maandamano kama hayo yanayoendelea katika jimbo la Magharibi ya Kati ya Marekani la Minnesota, kuhusu mauaji kwa risasi watu yaliyosababishwa na maafisa wa serikali kuu ya Marekani. Wakazi wawili waliuawa katika visa tofauti mwezi Januari wakati wa msako mkubwa wa utawala wa Rais Donald Trump ukiwalenga wahamiaji wasio na vibali.
Vyombo vya habari vya Marekani vinasema kwamba ICE iliwatuma maafisa wake kwenye Olimpiki zilizopita ili kusaidia katika usalama, na kwamba wafanyakazi watakaotumwa sio wanaoendesha shughuli za utekelezaji wa uhamiaji.
Ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wa mamlaka za serikali kuu ya Marekani mnamo Januari 27 ulisema, “Ni wazi kwamba, ICE haiendeshi shughuli za utekelezaji wa uhamiaji katika nchi za kigeni.”