Israel inasema kivuko cha mpakani cha Rafah kati ya Ukanda wa Gaza na Misri “kimefunguliwa tena kwa ajili ya watu pekee.” Inaongeza kuwa kupita kwa wakazi katika pande zote mbili kunatarajiwa kuanza Februari 2.
Israel ilitoa tangazo hilo Februari mosi. Kivuko hicho kilikuwa kimefungwa kutokana na shughuli za kijeshi za nchi hiyo.
Gazeti kubwa la Israel la Haaretz liliandika, “Katika hatua hii, ni Wapalestina wagonjwa na waliojeruhiwa pekee ndio wataruhusiwa kutoka Ukanda wa Gaza, pamoja na wale wanaoambatana nao.”
Pia linamnukuu afisa wa usalama wa Israel akisema kwamba watu kati ya 150 na 200 wanaoingia na kutoka wanatarajiwa kwenye kivuko hicho kila siku.
Mamlaka za afya huko Gaza zinasema takriban watu 20,000 katika ukanda huo wanahitaji matibabu nje ya eneo hilo kutokana na uhaba wa vifaa vya matibabu na dawa.
Umoja wa Mataifa unaitaka Israel kupanua zaidi matumizi ya kivuko hicho. Unataka nchi hiyo iruhusu vifaa vya misaada kusafirishwa hadi Gaza kupitia lango hilo.