Mjumbe wa Marekani Laura Dogu amewasili nchini Venezuela kufungua tena misheni ya kidiplomasia ya Marekani huko Caracas.
Shirika la Habari la Associated Press na vyombo vingine vya habari viliripoti kwamba Naibu Balozi Dogu aliwasili katika mji huo mkuu wa Venezuela Januari 31.
Hatua hiyo inaonekana kama sehemu ya juhudi za utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kuimarisha uhusiano na Venezuela chini ya Rais wake wa mpito Delcy Rodriguez.
Mnamo 2019, Rais Nicolas Maduro alitangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Marekani. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliwaondoa wafanyakazi kutoka ubalozi wake huko Caracas na kusimamisha shughuli zake.
Takriban mwezi mmoja umepita tangu utawala wa Trump ulipomkamata Maduro katika operesheni ya kijeshi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela Yvan Gil alielezea matumaini yake kwamba nchi hizo mbili zitatatua tofauti zilizopo kupitia mazungumzo ya kidiplomasia.