Majeshi ya nchi za Ulaya yamefanya jinai barani Ulaya na katika mabara mengine duniani katika karne chache zilizopita.
Kwa mujibu wa Press TV, majeshi ya nchi za Ulaya iwe wakati wa ukoloni, baada ya ukoloni na baada ya kipindi cha Vita Baridi yalifanya jinai nyingi za kigaidi katika mabara tofauti duniani. Yafuatayo ni simulizi zilizochaguliwa kutoka mabara 5 kuhusu suala hilo:
Simulizi ya kwanza ni kuhusu jinai za ugaidi zilizofanywa na jeshi la Uingereza katika kuivamia na kuikalia kwa mabavu Iraq kwa kushirikiana na Marekani mwaka 2003. Katika uvamizi huo ambao uliendelea hadi mwaka 2011, wanajeshi wa Uingereza walitenda jinai kubwa za kivita dhidi ya raia na watu wote waliokuwa wakitiwa mbaroni. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) mwaka 2017 ilitangaza kuwa “kuna “msingi wa kuridhisha” kwamba askari wa Uingereza wamefanya jinai ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso, ukatili na udhalilishaji wa kingono. Mateso hayo yalijumuisha vipigo vikali, kuzuiwa wafungwa kulala baada ya mateso makali, kutukanwa, kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini na katika baadhi ya matukio kudhalilishwa kingono. Licha ya kusajiliwa maelfu ya madai na kufanyika uchunguzi mkubwa wa ndani, mfumo wa haki wa Uingereza haukufuatilia kivitendo mashtaka yoyote ya uhalifu uliofanywa na majeshi ya nchi hiyo dhidi ya watu wa Iraq, hasa kuhusu makamanda wakuu, na uchunguzi ulimalizika bila kuadhibiwa. Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilitoa mamilioni ya pauni ili kutatua baadhi ya kesi hizo bila ya kukubali jukumu na kubeba dhima ya jinai zilizofanyika. Mchakato huo ni mfano unaotia wasiwasi sana kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wa madola yenye nguvu za kijeshi duniani bila ya kuwajibishwa ipasavyo.
Simulizi ya pili, mashambulizi ya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) hasa Marekani na Uingereza dhidi ya Yugoslavia hapo mwaka 1999. Hujuma na mashambulizi hayo yaliendelea kwa muda wa siku 78. Mashambulizi dhidi ya Yugoslavia yalikuwa hujuma ya kijeshi iliyofanyika bila idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Oparesheni hiyo iliyofanywa kwa madai ya kusitisha ukandamizaji dhidi ya Waalbania wa Kosovo ilisababisha maafa makubwa ya binadamu. Ripoti za kuaminika zinaeleza kuwa raia 489 hadi 528 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya NATO. Mashambulizi yaliyolenga treni ya abiria huko Gojna Gora huko Serbia, msafara wa wakimbizi huko Dakovica na kituo cha televisheni cha Redio ya Serbia (RTS) huko Belgrade, ambayo yalisababisha vifo vya raia yalikosolewa pakubwa kikanda na kimataifa. Kamati Maalumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Yugoslavia (ICTY) ilichunguza matukio hayo lakini hadi sasa hakua mashtaka yoyote rasmi yaliyofunguliwa dhidi ya maafisa wa NATO kuhusu jinai za Yugoslavia. Matokeo ya mwisho ya vita hivyo vilivyoambatana na mashambulizi makubwa yalikuwa kutenganishwa Kosovo na Serbia na kusababisha hasara kubwa na uharibifu wa miundombinu nchini humo.

Simulizi ya tatu, ni mashambulizi ya kijeshi ya NATO nchini Libya yaliyoanza Machi 19 hadi Oktoba 31 mwaka 2011, kwa jina la “Operation Unified Protector”. Mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuandaa eneo lisiloruhusiwa kuruka ndege la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Uvamizi huo ambao ulipelekea kuangushwa serikali ya Libya uliambatana na tuhuma nzito za kufanyika jinai na mauaji ya raia. Kwa mujibu wa ripoti za mashirika kama Human Rights Watch, mashambulizi ya anga ya NATO nchini Libya yaliuwa raia wasiopungua 72. Baadhi ya ripoti na taasisi ya utafiti ya ‘Airwars’ zinasema kwamba idadi ya raia waliouawa ni kati ya 223 hadi 403. Licha ya takwimu hizi, Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) hadi sasa umekataa kukubali na kubeba dhima au kuomba radhi rasmi na kuzilipa fidia familia za wahanga.
Wakosoaji kwa upande wao wanasisitiza kuwa licha ya madai kwamba mashambulizi hayo yalifanywa kuwalinda raia, yalikwenda mbali ya fremu yake ya awali na yalitumika kama wenzo wa kuondoa madarakani serikali ya nchi hizo, jambo ambalo lilisababisha kukosekana utulivu na migogoro ya muda mrefu nchini Libya.
Simulizi ya nne, ni jinai za jeshi la Uingereza wakati wa Vita vya Malaya au The Malayan War. Katika vita hivyo vilivyojiri kuanzia 1948 hadi 1960, wanajeshi wa Uingereza walifanya vitendo vya ukatili na jinai ili kuwakandamiza waasi wa Kikomonti ambapo mbinu ya decapitation yaani ya kukata vichwa ilikuwa mojawapo ya ukatili mkubwa wa Waingereza. Baadhi ya wanajeshi wa Uingereza walitumia njia hiyo kama mbinu ya mauaji ya kisaikolojia dhidi ya vijiji vilivyoshukiwa kuwaunga mkono waasi. Kashfa ya kukata vichwa ya Uingereza huko Malaya ilisajiliwa rasmi mwaka 1952. Malaya ya Uingereza ilikuwa sehemu ya majimbo ya Peninsula ya Malay na kisiwa cha Singapore, maeneo ambayo yalikuwa yakidhibitiwa na Uingereza mwishoni mwa karne ya 18 na katikati ya karne ya 20. Picha maarufu ya mwanajeshi wa Marrine Commando wa Uingereza mwezi Aprili 1952 inamuonyesha akitabasamu akiwa ameshikilia vichwa vilivyokatwa vya mwanamke na mwanaume vijana ambao walikuwa wakituhumiwa kukiunga mkono Chama cha Kikomunisti cha Malaya. Lengo la kitendo hicho lilikuwa kujenga hofu katika jamii na kuvunja uungaji mkono wa wananchi kwa waasi. Aidha imeripotiwa kuwa, baadhi ya nyakati walikuwa wakiwakata vichwa wapiganaji waliouawa ili kuwatambulisha. Waingereza waliwatumia hata wawindaji wa vichwa vya watu waliojulikana kwa jina la Dayak kutoka Borneo kwa ajili ya kazi hiyo. Watu wa Dayak walikuwa wapiganaji wakali ambao wakati fulani walijulikana kwa kazi ya kuwinda vichwa, kazi ambayo ilihusisha kukata kichwa cha adui na kukishikilia kama nyara.
Kitendo hicho cha kikatili, pamoja na ukatili mwingine kama vile mauaji ya Batang Kali (mauaji ya raia 24 wasio na silaha yaliyofanywa na Scotland Yard mwezi Desemba 1948) na adhabu za pamoja kama vile kuhamishwa kwa lazima kwa mamia ya maelfu ya watu kwenye kambi zinazojulikana kama “Vijiji Vipya”, ilikuwa sehemu ya mkakati wa kikatili wa Uingereza kwa lengo la kudumisha udhibiti wao wa rasilimali za bati na mpira za Malaya.
Mauaji ya Batang Kali yalikuwa mauaji ya raia 24 wa kiume wasio na silaha huko Batang Kali yaliyofanywa na Jeshi la Uingereza tarehe 12 Desemba 1948.
Simulizi ya tano uvamizi wa jeshi la Ufaransa katika nchi ndogo ya Haiti huko Amerika ya Latini. Mapambano ya watumwa wa Haiti, ambayo yalianza mwaka 1791 yalisababisha mapinduzi ya kwanza ya watumwa yenye mafanikio katika historia ya dunia na kufuatiwa na tangazo la uhuru wa nchi hiyo mwaka 1804. Mwaka1802, Mfalme wa Ufaransa, Napoleon Bonaparte, alituma jeshi kubwa la watu 40,000 hadi 60,000 chini ya amri ya Jenerali Charles Leclerc kwenda Haiti kwa lengo la kurejesha utumwa na kuidhibiti tena Haiti baada ya kutangaza kuwa huru. Jeshi la Ufaransa lilifanya ukandamizaji na umwagaji damu mkubwa na kuua maelfu ya watu. Hata hivyo mapambano makali ya Wahaiti wakiongozwa na Jean-Jacques Dessalines, yaliwasababishia maafa makubwa wavamizi kutokana na homa ya manjano; na kushindwa katika vita vya mwisho kuliwalazimisha Wafaransa kurudi nyuma. Pamoja na hayo, Ufaransa mwaka 1825 na baada ya kutishia kushambulia tena, iliilazimisha Haiti kusaini mapatano. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Haiti ilidaiwa na Ufaransa faranga za dhahabu milioni 150 sawa na karibu dola bilioni 21 za hii leo kama fidia. Haiti ililazimika kukopa benki za Ufaransa ili kulipa deni hilo la kulemaza. Deni hilo liliendelea kwa muda wa miaka 122 hadi kufikia mwaka 1948 na suala hilo liliathiri uchumi wa nchi hiyo, kusababisha umaskini wa kimfumo na kurudisha nyuma ustawi wa vizazi kadhaa vya baadaye.

Fidia hiyo ya kidhulma ni moja ya sababu kuu za matatizo ya kiuchumi yanayoisibu Haiti kwa muda mrefu sasa.