Mexico. Mwigizaji wa Apocalypto Gerardo Taracena amefariki dunia. Mkali huyu alikuwa mmoja wa wachezaji filamu na tamthilia walioibuka kutoka Mexico. Alizaliwa Machi 27, 1970, na kufariki Januari 31,2026 akiwa na umri wa miaka 55.
Safari yake ya sanaa ilianza kwenye tamthilia, akifanya kazi tangu miaka ya 1990. Alienda kusomea Sanaa ya Uigizaji katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Mexico (UNAM), na baadaye akawa mwanachama wa vikundi vya teatro kama Teatro Mito na kufuzu zaidi kupitia ngoma na tamthilia mbalimbali.
Taracena alionyesha kipaji chake cha kipekee ndani ya filamu. Alijulikana zaidi kimataifa kwa mara ya kwanza alipocheza katika filamu ya kimataifa ‘Apocalypto’ (2006) iliyoongozwa na Mel Gibson.
Baadaye, alijizolea sifa zaidi kupitia kazi zake nyingi kwenye filamu kama ‘The Violin’, ‘Man on Fire’, ‘Sin Nombre’, na ‘Saving Private Perez’, pamoja na kazi zake kwenye televisheni kama ‘Queen of the South’ na ‘Netflix’s Narcos: Mexico’.
Katika safari yake ya zaidi ya miaka 30, Taracena alipata heshima nyingi, ikiwa ni pamoja na uteuzi mara kadhaa kwenye Tuzo za Ariel (Ariel Awards), tuzo kuu za filamu nchini Mexico, akishuhudia ubora wake kama mwigizaji mwenye nguvu na anayeweza kuuvaa uhusika.
Habari za kifo chake zilizotolewa na Jumuiya ya Taifa ya Wakurugenzi wa Filamu Mexico zilisema kazi zake zitaendelea kukumbukwa na wasanii na watazamaji duniani kote.